Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari
kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa SADC sekta ya Kazi na Ajira utakaofanyika
tarehe 2 – 6 Machi, 2020 Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bw. Robert Masingiri (kulia) ni
Mratibu wa Kamati ya Habari – Maelezo Bw. Jonas Kamaleki.
Baadhi ya Waandishi wa Habari
wakifuatilia taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
(hayupo pichani) alipokuwa akiwapa taarifa ya Mkutano wa Mawaziri wa
SADC sekta ya Kazi na Ajira katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika
Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na
Ukuzaji Ujuzi Bw. Robert Masingiri akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa
Habari kuhusu Programu ya Mafunzo kwa Vitendo Mahala pa Kazi
(Internship) kwa vijana wakati wa mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.
Jenista Mhagama na Waandishi wa Habari.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
**************************
Na: Mwandishi Wetu
Mkutano wa Mawaziri wa Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) sekta ya Kazi
na Ajira unatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia tarehe 2 hadi 6
Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNICC) uliopo
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Mkutano na Waandishi wa
Habari alieleza kuwa Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ikiwa ni “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu”.
Waziri Mhagama amesema kuwa katika
Mkutano huo ambao kwa kiasi kikukubwa utawakutanisha Mawaziri
wanaoshughulikia masuala ya Kazi na Ajira, Wataalam na Vyama vya Waajiri
na Vyama vya Wafanyakazi kutoka Nchi Wanachama wa SADC na utakuwa na
lengo la kujadili masuala mbalimbali ya sekta ya Kazi na Ajira katika
Ukanda huo wa Afrika.
“Mkutano huu wa Mawaziri,
Wataalamu na Wadau wa Utatu wa Sekta ya Kazi na Ajira utatoa fursa ya
majadiliano ya pamoja kwa nchi wanachama wa SADC kuangalia utekelezaji
wa maazimio mbalimbali kuhusu masuala ya Kazi, Ajira, Vijana, Uhamaji wa
Nguvukazi na Hifadhi ya Jamii”, Alisema Waziri Mhagama.
Alieleza kuwa katika Mkutano huo
itazindua rasmi Programu ya Mafunzo ya Uzoefu kwa Wahitimu Mahala pa
Kazi (Intership) kwa vijana inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alieleza kuwa Programu hiyo ni
Mahususi kwa vijana wa Kitanzania waliohitimu vyuo mbalimbali hapa
nchini na inagharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Waajiri.
“Serikali iliamua kuanzisha
Programu hii kwa lengo la kuwapatia fursa vijana ya kupata uzoefu,
ujuzi, maadili ya kazi na namna bora ya kuhudumia wateja katika sehemu
zao za kazi,” alieleza Mhagama
“Vijana 5,000 wameweza kunufaika
na programu hiyo na kati yao vijana wapatao 1,000 waliomaliza muda wao
wa mafunzo hayo wameweza kupata ajira katika maeneo mbalimbali,” alisema
Mhagama
Akitaja manufaa ya Programu hiyo
ya Mafunzo kwa Vitendo Mahala pa Kazi kwa Vijana kuwa ni pamoja na
Kuwawezesha vijana wanaoshiriki kuoanisha ujuzi waliopata kwenye taasisi
za elimu na mafunzo pamoja na mahitaji halisi ya ujuzi kwa waajiri;
Kuwezesha vijana kujifunza maadili, mtazamo chanya kuhusu kazi pamoja na
tamaduni za kuishi mahali pa kazi na Kuwapatia uzoefu wa kazi
unaohitajika na waajiri.
Aliongeza kuwa Programu hiyo
imeongeza ushirikiano mzuri kati ya waajiri, Serikali na Vijana na
imewapa hamasa waajiri kushiriki katika kuwajengea Ujuzi vijana, maadili
na weledi unaohitajika katika soko la Ajira.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito
kwa Wananchi ikiwemo wamiliki na Wafanyakazi wa Mahoteli, Migahawa,
Vyombo vya Usafiri na sehemu mbalimbali watakazotembelea wageni
kuwakarimu na kutoa ushirikiano na ukaribisho unaostahili ili sifa ya
nchi iendelee kuwa kielelezo kwa wageni.
No comments :
Post a Comment