Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua kituo cha dharura cha kuwapokea na kuwafanyia uchunguzi watu
wanaoingia nchini kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga ambao
wataonyesha kuwa na dalili za kuumwa magonjwa ya kuambukiza. Wa tatu
kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu na wa pili kushoto ni Naibu Waziri Nchi, Ofisi y Rais
TAMISEMI, Mwita Waitara. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Mbunge wa Mkinga, Danstan Kitandula wakati alipofungua
jengo la Ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Mkinga na kuzungumza na
watumishi wa Halmashauri hiyo, Machi 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Wananchi wakimsikiliza Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao baada ya kufungua jengo
la Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, Machi 2, 2020. (Picha
na Ofisi ya Waziri. Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitoka kwenye jengo la Kituo cha Pamoja cha Huduma za Forodha cha
Horohoro mkoani Tanga wakati alipokitembelea kituo hicho, Machi 2, 2020.
Kulia kwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
****************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa jengo la kituo cha
pamoja cha huduma ya forodha kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya
eneo la
Horohoro, Tanga ambacho ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 7.6.
“Jengo hili kuta
tayari zimeshaanza kuvimba, kwa nini majengo ya TRA (Mamlaka ya Mapato
Tanzania) yanajengwa kwa kiwango cha chini na kwa nini mmeruhusu majengo
haya yatumike,” amehoji Waziri Mkuu.
Kufuatia hali
hiyo Waziri Mkuu amemtaka Afisa Miliki wa TRA, Bw. Haruna Sumwa,
mkandarasi aliyejenga jengo hilo pamoja na wote waliohusika na ujenzi
huo wafike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma Machi 11, 2020.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akiwa katika
ziara ya kikazi wilaya ya Mkinga mkoani Tanga. Amesema ni lazima majengo
hayo yakidhi viwango.
“Hapa ni sura ya
nchi ni lazima majengo yawe katika hali nzuri, haiwezekani mgeni
anaingia na kuhudumiwa katika jengo chakavu, tutachukua hatua kwa yeyote
aliyehusika, hizi ni fedha za umma lazima zitumike vizuri.”
Awali, Mkuu wa
wilaya ya Mkinga Bw Yona Maki alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza Julai
2011 hadi Septemba 2014 na lilianza kutumika Agosti 2015 likiwa na
taasisi 16 za Serikali zinazofanyakazi.
Mkuu huyo wa
wilaya alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
ukosefu wa nyumba 62 za watumishi, maji safi na salama pamoja na
upungufu wa watumishi.
Majukumu ya kituo
hicho ni pamoja na kusimamia, kudhibiti uingiaji na utokaji wa raia wa
Tanzania na wageni, kufanya doria na misako hasa kwenye vipenyo ambako
wale wasiopenda kufuata taratibu hupenda kutumia.
Wakati huo
huo,Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza watu wote wanaoingia nchini
kupitia mipaka mbalimbali wapimwe afya zao ili kulikinga Taifa na
maambuki ya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya mapafu inayosababishwa
na virusi vya corona.
Pia amewataka
wananchi kutoa ushirikiano na Serikali kwa kutoa taarifa za watu
wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu. “Lazima tulinde nchi yetu
katika kupambana na kuzuia magonjwa mbalimbali kwa kuhakikisha watu wote
wanaingia nchini wawe salama.”
Pia, Waziri Mkuu
amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Tanga kuimarisha doria
katika maeneo ya mpakani ikiwa ni pamoja na kukagua maroli kwa kuwa
yanahusika na ubebaji wa wahamiaji haramu.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amewataka wananchi kutojihusisha na biashara haramu ya dawa
za kulevya kwa kuwa madhara yake ni makubwa kwa jamii na Taifa kwa
ujumla.
Amesema wananchi
wakatae kutumika katika kupitisha dawa za kulevya na atakayekamatwa
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. “Usikubali gari lako
likatumika kubeba wahamiaji haramu wala dawa za kulevya kwani ukikamatwa
linataifishwa.”
Waziri Mkuu
amesema mwaka jana dawa za kulevya aina ya heroine gramu 746, bangi kilo
485, mirungi kilo 880 zilipitishwa katika wilaya hiyo kiawango ambacho
ni kikubwa, hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya aimarishe doria.
Kwa upande wake,
Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula alitaja changamoto
zinazoikabili wilaya hiyo ikiwemo ya ukosefu wa maji safi na salama,
ambapo Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imeshaanza
kushughulikia suala hilo.
No comments :
Post a Comment