……………………………………………………………………………………………………….
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam limemuhoji Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, JOSEPHAT
GWAJIMA kwa tuhuma za kusambaza kipeperushi na sauti kwa lugha ya
kisukuma zenye lengo la kuhamasisha watu kuunda kikundi cha kikabila
nchini.
Kipeperushi hicho chenye picha ya
rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimesambaa kwenye mitandao ya
kijamii kikiwa na maandishi yanayosomeka kwa lugha ya kisukuma.
Sambamba na kipeperushi hicho,
askofu Gwajima pia ametoa ujumbe wa sauti wenye ujumbe wa kumpongeza
mhe. Rais na kuhamasisha wasukuma kurejesha utamaduni wao wa zamani wa
kutumia lugha yao, kusaidiana katika shida na raha na kuwataka wasukuma
kuunda vikundi kwenye mitandao ya kijamii vya watu elfu mbili (2000) kwa
lengo la kufuatilia watu wanaomtukana mhe. Rais na kuwashughulikia.
Katika ujumbe huo wa sauti askofu
Gwajima pia amewataka wasukuma matajiri kuungana kwa pamoja kwa lengo la
kuwasaidia wasukuma masikini ili kuondoa dhana ya kwamba wasukuma ni
masikini na ni washamba.
Kufuatia jumbe hizo, Jeshi la
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemuhoji askofu Gwajima kutokana
na jumbe hizo kuonekana kuhamasisha vitendo vya kikabila jambo ambalo
linaweza kuwagawa watanzania na kupelekea kuvunjika kwa amani na
mshikamano wa nchi utakaotokana na uwepo wa matabaka ya kikabila.
Baada ya mahojiano hayo, Jeshi la
Polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam limemuonya askofu Gwajima kuacha
mara moja vitendo vya kuligawa taifa kwa kutumia vigezo vya ukabila na
kutoa onyo kwa wote wenye nia ya kutaka kuligawa taifa kwa njia ya
ukabila, udini au ukanda. Jeshi la Polisi halitamuonea muhali mtu yeyote
atakayebainika kujihusisha na vitendo vya aina hiyo na hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi kuendeleza umoja na mshikamano
uliopo nchini bila kujali dini, kabila wala rangi ya mtu kama ambavyo
baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyopinga vitendo vya
kibaguzi na kutuunganisha kuwa wamoja kwa lugha ya Kiswahili.
CAMILLIUS M. WAMBURA – SACP
KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM.
03/03/2020
No comments :
Post a Comment