Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akimuhoji mmoja wa
wahamiaji haramu waliokamatwa wilayani Misenyi, mkoani Kagera wakiingia
nchini kinyume na utaratibu ambapo ameitaka Idara ya Uhamiaji na Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuongeza nguvu kazi katika wilaya
hiyo ili kuweza kutambua raia wenye uhalali wa kuishi nchini.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mkuu wa Uhamiaji
Wilaya ya Misenyi,Inspekta Ferouz Lwambano, akimuonyesha Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni,mmoja wa wahamiaji
haramu aliyekamatwa tena baada ya kutoka kifungoni kwa msamaha wa Rais
Dkt, John Pombe Magufuli aliposamehe wafungwa wakati wa sherehe za
uhuru.Wahamiaji haramu hao wako ofisi za Uhamiaji Misenyi wakisuburi
taratibu za kisheria ili waweze kupelekwa mahakamani.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Baadhi wa
Wahamiaji Haramu waliokamatwa wilayani Misenyi, wakimuangalia Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni. Wahamiaji
haramu hao wako ofisi za Uhamiaji Misenyi wakisuburi taratibu za
kisheria ili waweze kupelekwa mahakamani.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mkuu wa Uhamiaji Wilaya ya
Misenyi, Inspekta Ferouz Lwambano, akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni baada ya
kuwaona Wahamiaji haramu waliohifadhiwa Ofisi za Uhamiaji Misenyi
wakisuburi taratibu za kisheria ili waweze kupelekwa mahakamani.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*****************************
Na Mwandishi Wetu,Misenyi
Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni ameitaka idara ya
uhamiaji
na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA),kuongeza nguvu kazi katika
Wilaya ya Misenyi baada kugundulika uwepo wa wahamiaji haramu wengi
wanaotishia hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Kagera unaopakana
na nchi za Uganda na Rwanda.
Ameyasema hayo
baada ya kusikiliza taarifa ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya
ya Misenyi iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,Kanali Denis Mwila
iliyoweka wazi idadi ya asilimia 95 ya wakazi katika Kata ya Kakunyu
iliyopo Wilayani Misenyi Mkoani Kagera ni wahamiaji haramu huku sababu
kubwa zikitajwa za ongezeko hilo ni kuletwa kwa wahamiaji hao kutafuta
ajira na kutafuta mashamba ya maeneo ya malisho ndani ya Ranchi ya
Taifa.
“kuna haja ya
kuleta nguvu kazi kubwa sana kutoka idara ya uhamiaji na NIDA,lazima
tuwe na takwimu halisi ya kila mtu aliyeko katika maeneo haya ambayo
yana mashaka,nchi yetu inakaribia kufanya uchaguzi mkuu ndani ya mwaka
huu,tunahitaji kuwa salama ili kuweza kufanya uchaguzi pasina shaka
yoyote ya uvunjifu wa amani ,tatizo hili ni kubwa linahitaji utatuzi wa
haraka ili kuepuka madhara huko mbeleni” alisema Masauni
Akitoa taarifa ya
idara ya uhamiaji kwa kipindi cha Januari hadi Disemba, 2019, Mkuu wa
Wilaya ya Misenyi, Kanali Denis Mwila, alisema idara ilitoa hati ya
dharura za kusafiria 1,276 zenye thamani ya Shilingi 25,520,000/- huku
makusanyo hayo yakikisiwa kuwa ni wastani wa makusanyo 2,126,666/- kwa
mwezi huku idara ikikamata wahamiaji haramu 206 kwa kipindi cha mwezi
Januari mpaka Disemba,mwaka jana.
“Tumekua na
matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika wilaya yetu mfano
katika kata ya Kakunyu watu 6,630 walisajiliwa huku raia halali wakiwa
319 tu,hivyo takribani asilimia 95 ya wakazi hao sio raia au uraia wao
una mashaka,wahamiaji hao ni gharama kuwahudumia maana bado wana haki ya
kuhifadhiwa na kupata mahitaji yote ya kibinadamu” alisema Kanali Mwila
Wakizungumza
mbele ya Naibu Waziri wahamiaji hao waliomba kupatiwa nauli ili warejee
katika nchi zao huku wengine wakitaja sababu ya kuingia nchini kinyume
na sharia ni kuja kutafuta ajira na kukimbiwa na wenza wao.
No comments :
Post a Comment