Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony (mbele) akikagua chanzo cha maji cha mradi wa Longido
katika Mto Simba uliopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro ili kutazama
uwezekano wa kutoa maji kwenye chanzo hicho na kupeleka Namanga.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony (katikati) akitoa maelekezo kwa wataalam kutoka Mamlaka
ya Maji Arusha (AUWSA) wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi
wa maji wa Longido. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA,
Mhandisi Justine Rujomba

Naibu katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony (kushoto) akitoa maelekezo kwa
wataalam kutoka Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) wakati wa ziara yake ya
kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa Longido.
**************************************
Mamlaka ya Maji
Arusha (AUWSA) imetakiwa kuharakisha zoezi la tathmini ya kupeleka
huduma ya maji katika Mji wa Namanga ili kusaidia wananchi kuondokana na
changamoto ya upatikanaji wa maji.
Agizo hilo
limetolewa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga
wakati wa ziara yake kwenye chanzo cha mradi wa maji wa Longido katika
Mto Simba uliopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro Novemba 4, 2019 kwa
lengo la kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wake.
Mhandisi
Sanga alisema ameridhika na hatua aliyoishuhudia ya ujenzi wa mradi wa
Longido hata hivyo aliitaka AUWSA kuhakikisha inatazama namna ya haraka
ya kufikisha huduma ya maji kwenye mji wa Namanga kutoka kwenye chanzo
cha mradi huo hasa ikizingatiwa kwamba mji huo unasumbuliwa na kero ya
upatikanaji wa huduma ya maji.
“Ninawapongeza
AUWSA kwa usimamizi mzuri wa mradi lakini nataka kuona mnafanya
tathmini haraka ya namna ya kufikisha maji kwenye mji wa Namanga kwani
kuna changamoto kubwa sana kwenye mji huo,” alisema Mhandisi Sanga.
Akizungumzia
uwezekano wa kutumia chanzo hicho cha Mto Simba kupelekea maji Namanga,
Mhandisi Sanga alisema maji yaliyopo yanaonekana kuwa mengi na yanaweza
kutosheleza kuhudumia maeneo yote mawili sambamba na maeneo mengine ya
jirani.
“Tumekuja
hapa kuona uwezekano wa kutoa maji kwenye eneo hili ili kufikisha
Namanga, na nilichoshuhudia ni kwamba chanzo hiki kinaonekana kuwa na
maji ya kutosha kwa maeneo yote mawili yani Longido na Namanga,”
alisema.
Aliwataka
kufanya mawasiliano ya haraka na Bonde la Pangani ili kuharakisha zoezi
la tathmini ya kuona kiasi cha maji kinachoweza kuongezwa ili kuwezesha
kupeleka maji kwenye mji wa Namanga kutoka kwenye chanzo hicho bila
kuathiri matumizi ya asili ya chanzo hicho.
Kwa upande
wake kaimu Mkurugenzi wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba alisema mradi
wa Lingido umelenga kuongeza upatikanaji wa maji katika mji mdogo wa
Longido kutoka asilimia 15 za sasa ambazo ni sawa na wananchi 2,510 hadi
kufikia asilimia mia moja ambayo ni sawa na wananchi 16, 712.
Mhandisi
Rujomba aliongeza kuwa malengo hayo ni hadi kufikia mwaka 2025 na kwamba
hadi kukamilika kwake utakuwa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni
15.8. Aidha aliongeza kuwa wamepokea maagizo ya Naibu Katibu Mkuu na
wanaanza kufanyia kazi maramoja.
Mhandisi
Sanga yupo Mkoani Arusha akiendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya
maji inayotekelezwa mkoani humo kwa lengo la kujionea hali halisi ya
utekelezaji sambamba na kuelewa changamoto zilizopo ili kuzipatia
ufumbuzi wa haraka.
No comments :
Post a Comment