Monday, July 1, 2019

UJANGILI WAPUNGUZA IDADI YA FARU KUTOKA ZAIDI YA ELFU 10 HADI 161 PEKEE


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Imeelezwa kuwa  idadi ya wanyamapori aina ya  Faru weusi[Black Rhino]   imepungua kutoka faru   zaidi ya elfu  kumi kwa miaka 1970 mpaka 1980 na  kubaki faru   161 pekee  hadi sasa hapa nchini  kutokana na Ujangili.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Dokta  Hamis Kigwangalla wakati akizindua mpango kazi  wa kulinda na kutunza Faru weusi uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Dokta Kigwangalla amesema kutokana na tishio kubwa la faru kutoweka hapa nchini kwa sababu ya   ujangili, serikali imeandaa mikakati kabambe ya kudhibiti ujangili hali ambayo imeanza kuzaa matunda na kuanza kusababisha faru kuongezeka  ambapo  serikali imetenga Dola milioni 61 sawa na zaidi ya Tsh.Bilioni 120 za kitanzania  kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo.
Aidha,Dokta Kigwangalla amesema sekta ya  utalii hapa nchini  huzalisha zaidi ya Dola za Marekani bilioni 2  ambazo huchangia asilimia 25%  ya fedha za kigeni  na kuchangia asilimia 17% ya mapato ya ndani ya nchi [GDP ]  na imetoa ajira rasmi laki sita[600,000]  na zisizo rasmi milioni mbili[2000,000] hivyo ulinzi wa wanyamapori  walio katika hatari ya kutoweka wakiwemo faru utaendelea kuimarishwa  na mpango wa serikali ni kuhakikisha  uzalishaji wa faru unaongezeka kwa kasi kwa miaka mitano ijayo.
Katika hatua nyingine ,Dokta Kigwangalla ameitaka jamii kuachana na mila potofu za kutumia pembe za faru kama  dawa za kuongeza nguvu za kiume kwani imani hizo hazina ukweli wowote na zinapaswa kupuuzwa.
Mtafiti kutoka   taasisi ya utafiti ya wanyamapori nchini,TAWIRI Dokta Edward Kohi  amesema kunahitaji teknolojia zaidi ili kuhakikisha faru anatunzwa   ambapo miaka ya 1998 waliingia kwenye tatizo la kutoweka hadi sasa kuna faru 161 wanaoweza kuhesabiwa na kuonekana.
Pia  ,Dokta Kohi ametaja malengo madhubuti ya  Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania,[TAWIRI ] ni Pamoja   kuongeza idadi ya faru si chini ya 5%  kwa mwaka,kuwa na uwezo wa kuhamisha faru kutoka eneo  moja hadi jingine,kuhakikisha ujangili wa faru uwe chini ya 1%     pamoja na kuwa na mfumo wa mawasiliano na mipaka mingine.
Naye mwakilishi kutoka  mfuko wa wanyamapori ulimwenguni[WWF] Dokta  Simon Lugandu amesema mradi wa kuhifadhi na kutunza  faru Tanzania unaendelea   katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira ‘
Ikumbukwe kuwa Tanzania ilishaanza   kutumia teknolojia ya kufuatilia faru ambapo mradi wa teknolojia hiyo ya kifaa chenye uwezo  wa kutoa  maelezo mwenendo wa faru  ,unagharimu dola za kimarekani 111,320  na unatekelezwa kwa ushirikiano na maafisa wa TANAPA ,Maafisa wa Shirika  la Wanyama la Frankfurt[FZS]na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania[TAWIRI]

No comments :

Post a Comment