
Mwili wa aliyekuwa Meneja Mawasiliano wa
Shirika la Kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi kwa Watoto na Familia (Agpahi),
Agnes Kabigi, aliyefariki dunia akiwa kazini wilaya ya Kahama, mkoani
Shinyanga utazikwa kesho Jumanne Julai 30,2019 katika makaburi ya Bahari
Beach kwa Kondo Goba, Dar es Salaam.
Agnes ambaye kitaaluma ni mwandishi wa
habari mwandamizi alifariki dunia Ijumaa wiki iliyopita mchana baada
kuanguka ghafla wakati akitekeleza majukumu yake akiwa katika hospitali
ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Mwili wake uliagwa juzi mkoani humo na kusafirishwa hadi jijini Dar es salaam kwa ajili ya maziko.
Katika uhai wake Agnes aliwahi kufanya
kazi katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Nipashe na wakati mauti
yanamkuta alikuwa anafanya kazi katika shirika la Agpahi ambalo
linafanya shughuli zake katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu na
Mara.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa
shirika la Agpahi wakati wa kuaga mwili wa marehemu, mfanyakazi wa
shirika hilo mkoa wa Shinyanga, Kasablankhahr Herman, alisema wakati wa
uhai wake, Agnes alikuwa mfanyakazi mbunifu na mwenye uwezo wa hali ya
juu hasa katika kutekeleza majukumu yake.
“Alikuwa ni mfanyakazi ambaye hakuna mtu
aliyechoka kufanya naye kazi, alikuwa na uwezo wa kazi na aliipenda
kazi yake, hakika ni pigo kubwa kwenye shirika na pia nitoe pole kwa
tasnia ya wanahabari,” alisema.
Akizungumza na gazeti la Habarileo,
mwanahabari, Beatrice Bandawe aliyewahi kufanya kazi na marehemu katika
gazeti la Nipashe alisema Agnes alikuwa mchapakazi aliyeipenda kazi yake
huku akiongozwa na misimamo dhabiti hasa katika kusimamia maadili ya
kazi.
“Ninakumbuka mwaka 1996 ninajiunga na
Nipashe, Agnes ndio alinipokea na alikuwa akinifundisha na kuniongoza
katika kazi, hakika ni pigo kwa tasnia kwa kuondokewa na mkongwe mahiri
katika fani kama huyu,” alisema.
Chanzo - Habarileo
No comments :
Post a Comment