NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
WADAU wa sekta ya
afya wameaswa kuimarisha ubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP)
mkoani Pwani, badala ya kusigana kwenye baadhi ya mambo ili kujiepusha
kuweka rehani maisha ya wananchi ambao wanahitaji huduma bora ya afya .
Akitoa rai hiyo,
wakati wa kikao kilichowakutanisha pande hizo mbili mjini Kibaha, mkuu
wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo aliwaambia afya ni kitu
muhimu kwenye maisha ya binadamu ili aweze kushiriki katika shughuli za
kimaendeleo hivyo waondoe tofauti, kila mmoja kwa nafasi yake awe sehemu
yake ili kutoa huduma.
Alieleza ,mkoa huo
una jumla ya vituo vya kutolea huduma ya afya 342 ,kati ya hivyo 275 ni
vya umma, 33 binafsi na 34 vya mashirika ya dini lakini ni vituo 20
vyenye malengo ya kuingia mkataba wa utoaji huduma ambapo sita pekee
ndio vilivyoingia mkataba.
“Kutokana na hali
hii, manake kuna baadhi ya maeneo yanaathirika kwenye utoaji huduma
kutokana na kutokuwa na makubaliano ya sekta ya umma na binafsi
“anasema.
Ndikilo alifafanua,
asilimia 20 ni vituo vya binafsi mkoani humo na asilimia 80 ni vya umma
hivyo bado kuna umuhimu wa kushirikiana ili kuboresha huduma hizo.
Aidha aliwataka wadau hao, kukutana kila mwaka ili kutathmini, kusimamia utekelezaji na mwenendo wa ubia baina ya sekta hizo.
Nae mratibu wa ubia
kati ya sekta ya umma na sekta binafsi Pwani, Dk. Hussein Athuman
alibainisha lengo la kukutana ni kujenga mahusiano baina ya pande hizo,
kubadilishana uzoefu na kujiwekea mikakati itakayosaidia kuleta chachu
ya mabadiliko chanya kwenye sekta ya afya.
Awali Dk. Mariam
Ongara kutoka wizara ya afya alielezea, vituo vya kutolea huduma ya afya
binafsi na mashirika ya dini vina mchango mkubwa kwa jamii.
Mariam alisisitiza serikali inatambua mchango unaotolewa na sekta binafsi kwani ina mchango mkubwa kwa watanzania.
No comments :
Post a Comment