Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasha Mwenge kuashiria
kuzinduliwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Mlowo mkoani
Songwe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mwenge
kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali
kutoka Mjini Magharibi kuashiria kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru
2019.
Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
……………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa
Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutumia mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka huu 2019 kumkumbuka Baba wa Taifa kwa kupinga vitendo
vya
dhulma, ufisadi, rushwa, maradhi, chuki, dharau na kuwataka kuenzi
umoja na mshikamano wetu kuchapakazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo
kwenye sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa zilizofanyika
kwenye uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
“Nimependezwa na kaulimbiu hii
ambayo inauwiano wa moja kwa moja na jukumu langu la kila siku la
kusimamia na kutunza mazingira ya nchini. Sote tunafahamu kuwa bila
utunzaji thabiti wa mazingira basi vyanzo vya maji hupotea”alisema
Makamu wa Rais
Hali ya upatikanaji wa huduma ya
maji safi na salama nchini inaendelea kuimarika ambapo huduma ya maji
vijijini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 58.7 kwa mwaka 2018
hadi kufikia asilimia 64.8 mwezi februari 2019 na miji mikuu ya mikoa
kutoka asilimia 78 mwezi machi 2018 mpaka asilimia februari 2019.
“Niwahakikishie wananchi
tutatekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi
inayotutaka kuboresha huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 85 na
mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2020”alisisitiza Makamu wa Rais
Aidha, Makamu wa Rais kupitia
hadhara ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019 ametoa
wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kufanya
shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, ukataji na
uchomaji miti kwenye vyanzo vya maji.
Makamu wa Rais pia amewakumbusha
wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwezi oktoba
2019 kuhakikisha wanachagua Viongozi wachapakazi na wenye dhamira ya
maendeleo kwa jamii.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 zitaongozwa na Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi
No comments :
Post a Comment