Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Amon Mpanju ( katikati) akitoa maagizo nje ya gereza la
Wanawake la WIlaya ya Musoma baada ya kutembelea gereza hilo kwa ajili
ya kufanya ukaguzi na kuzungumza na wafungwa na mahabusu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Amon Mpanju ( alieshika fimbo nyeupe) ikiwa katika picha
ya pamoja na timu ya wataalamu nje ya gereza la Wilaya ya Musoma mkoani
Mara baada ya kufanya ukaguzi ndani ya gereza hilo na kuzungumza na
wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Amon Mpanju ( alieshika fimbo nyeupe) ikiwa katika picha
ya pamoja na timu ya wataalamu nje ya gereza la Wilaya ya Tarime mkoani
Mara baada ya kufanya ukaguzi ndani ya gereza hilo na kuzungumza na
wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
(DPP) Bw. Biswalo Mganga (katikati ya Maaskari Magereza) katika picha ya
pamoja na timu ya wataalamu nje ya gereza la Wilaya ya Mugumu-
Serengeti mkoani Mara baada ya kufanya ukaguzi ndani ya gereza hilo na
kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo na
kuwaachia huru mahabusu 66.
………………………
Mahabusu 201 waliokuwa katika
magereza ya Wilaya za Musoma, Tarime na Mugumu Serengeti wamefutiwa kesi
zao mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili kufuatia ziara ya ukaguzi ndani
ya magereza hayo ya mkoa wa Mara iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya
Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
(DPP) Bw. Biswalo Maganga mwishoni mwa wiki iliyopita.
Viongozi hao walioambatana na
wataalamu wao walifanya ukaguzi ndani ya magereza na kuzungumza na
wafungwa na mahabusu walioko ndani ya magereza hayo nao ili kujua
changamoto za kisheria zinazowakabili na kuchukua hatua mbalimbali ili
kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinatatuliwa.
Baada ya kuzungumza na
mahabusu hao na kupitia majalada yao Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.
Biswalo Mganga aliwaagiza waendesha mashtaka mkoa wa Mara kwenda
Mahakamani na kuzifuta kesi zilizokuwa zikiwabili mahabusu hao ambao
wataachiwa huru baada ya Mahakama kupokea nia ya DPP ya kufuta kesi hizo
kwa mujibu wa sheria.
Mahabusu hao 29 wanatoka
katika Gereza la Wilaya ya Musoma, 106 wanatoka katika Gereza Tarime na
wengine 66 wanatoka katika Gereza Mugumu-Serengeti.
Katika Mahabusu hao wanawake
ni 11, Watoto 39, wazee 9 na wanaobakia ni vijana ambao walikuwa
wakikabiliwa na kesi mbalimbali ambazo zilionekana zinaweza kumalizwa
nje ya Mahakama, zile ambazo ushahidi wake ulionekana kuwa hafifu, kesi
ndogo ndogo kama kupigana, kutukanana, wizi wa simu na vitu vingine
vidogo vidogo, kutishiana kwa maneno, waliokiri kunywa gongo na kuvuta
bangi, wengine walionekana kuwa mashahidi wa mashtaka.
Akizungumza na wafungwa na
mahabusu katika nyakati tofauti ndani ya magereza hayo Naibu Katibu Mkuu
Bw. Mpanju aliwataka mahabusu watakaofutiwa Mashtaka yao kubadili
mienendo yao na kuwa raia wema na kuacha kuishi kimazoea kwani kufanya
hivyo ni kuvunja sheria na Serikali haitoacha kuwachukulia hatua za
kisheria.
“Ndugu zanguni mmeona kazi
kubwa tulioifanya leo hii humu ndani, ni wajibu wenu kuwa raia wema na
kubadili mienendo ya maisha yenu, muache kuishi kwa mazoea, muangalie
mnavyoishi na mkiachiliwa mkaambie na wenzenu kwani kufanya hivyo ni
kuvunja sheria na Serikali haitawaacha lazima hatua za kisheria
zichukuliwe”, alisema Bw, Mpanju.
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka
nchini (DPP) ambaye ni mratibu wa upelelezi wa kesi za jinai nchini Bw.
Biswalo Mganga aliwataka wote wanaohusika na kazi ya upelelezi wa kesi
mbalimbali zinazowakabili mahabusu hao kuhakikisha wanakamilisha
upepelezi wa kesi mbalimbali kwa wakati ili kuondoa hali ya upelelezi
kuchelewa.
Amesema kitendo cha
kuchelewesha upelelezi kinawafanya watuhumiwa wa makossa ya jinai nchini
kukaa magerezani kwa muda mrefu bila ya kujua hatma zao na hivyo
kufanya magereza kuwa na msongamano ambao unaweza kuzuiliwa.
“Wapelelezi mlioko hapa,
nadhani mnaelewa ninacho kisema hapa, fanyieni kazi haraka kesi za
watuhumiwa hawa ili ziweze kumalizwa na wajue moja kama wanafungwa au
wanaachiwa huru maana kwa kuendelea kuwa mahabusu hakuna tija kwa taifa,
hawa watu humu ndani wanatakiwa wafanye kazi za uzalishaji na hiyo
inakuwa sehemu ya urekebishwaji na sio kukaa bure na kujazana”, alisema
Bw. Mganga
Mahabusu hao walikabidhiwa kwa
mkuu wa upelelezi mkoa wa Mara ili kuhakikisha wanarudisha vitu
walivyoiba, wanaombana misamaha na kuwa raia wema ndani ya jamii zao na
kuambiwa kuwa Serikali itawachukulia hatua za kisheria tena iwapo
wataenda uraiani na kujihusisha na vitendo vya kihalifu.
Katika ziara hiyo Naibu Katibu
Mkuu Mpanju aliongozana na wataalamu wa Sheria kutoka Wizara ya Katiba
na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Taifa akiwemo Naibu
Mkurugenzi wa Mashtaka Dkt. Edson Makallo na Mkoa wa Mara, Maafisa
kutoka Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Waendesha Mashtaka kutoka
TANAPA.
No comments :
Post a Comment