Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba (katikati) akiongea na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na
Mazingira Mhe. Suleiman Murad Sadick katika moja ya ziara za kikazi za
Kamati hiyo hivi karibuni.
………………..
Na Lulu Mussa,Dodoma
Serikali imesema itaendelea na
juhudi za kushawishi wadau wa maendeleo na Jumuiya za Kimataifa ili
kupata fedha za kusimamia uratibu wa shughuli za mazingira na
kukabiliana na
Athari za Mabadiliko ya Tabianchi nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameyasema hayo hii leo
Jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na
Bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Makadirio ya Mapato na Matumizi
kwa mwaka 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara
na Mazingira. Amesema Tanzania ni Mwanachama kwenye Mifuko na Mikataba
mbalimbali duniani hivyo kuna fursa za kunufaika na fedha zitolewazo na
mifuko hiyo akitoa mfano wa Green Climate Fund.
Aidha Waziri Makamba ameainisha
mafanikio yaliyopatikana katika Ofisi yake kwa kipindi cha mwaka
2018/2019, kuwa ni pamoja na kufanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya
Mazingira ya mwaka 1997 na Mkakati wa Utekelezaji wake, kuandaa rasimu
ya Mpango wa Taifa wa Mazingira wa mwaka 2019 – 2023, na Maandalizi ya
Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi (Invasive Alien Species).
Pia, katika kipindi cha mwaka
2018/19, Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha rasimu ya mwisho ya Ripoti
ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini baada ya kupata maoni ya wadau
kabla ya kuwasilishwa Bungeni kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya
Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.
Waziri Makamba amesema katika
kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira unazingatiwa
jumla ya miradi 1,254 ya maendeleo imefanyiwa Tathmini ya Athari kwa
Mazingira (TAM) na Ukaguzi wa Mazingira na katika kuharakisha uwekezaji
katika sekta ya viwanda nchini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira linatoa Kibali cha Awali cha Mazingira (Provisional
Environmental Clearance) ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na
maandalizi ya awali ya mradi wakati mchakato wa Tathmini ya Athari kwa
Mazingira unaendelea.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Sadick
amepongeza uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa jitihada za kuhifadhi
mazingira nchini. ” Kamati inatambua jitihada za Ofisi yenu katika
kuhifadhi mazingira, sisi tunawaunga mkono” alisisitiza Mhe. Sadick.
No comments :
Post a Comment