Zao la Korosho katika kipindi
kilichoishia Januari 2018 liliingizia Taifa fedha za kigeni shilingi
1,136,609,586,722 ikilinganishwa na mazo mengine ya biashara.
Akijibu swali la Mbunge wa Mtwara
Mjini, Mhe. Maftaha Abdallah Nachuma, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.
Omari Mgumba, amesema licha mchango huo katika uchumi wa Taifa, zao la
korosho limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo Serikali
imekuwa
ikizitafutia ufumbuzi ikiwemo kuongeza bei ya korosho na
kutafuta masoko ya uhakika.
Mhe. Mgumba amezitaja changamoto
hizo kuwa ni kuyumba kwa bei ya korosho katika soko la dunia kutokana na
zao hilo kuuzwa likiwa ghafi yaani bila kuongezwa thamani, tija ndogo
katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kutotumia miche bora na matumizi
hafifu ya pembejeo ikiwemo viuadudu kama salfa na wakulima kutozingatia
kanuni bora za kilimo katika uzalishaji.
Aidha, Mhe. Mgumba amezitaja
changamoto nyingine kuwa uvunaji na uhifadhi hafifu wa korosho, uwezo
mdogo wa maghala ya kuhifadhia korosho na baadhi ya wakulima kuchanganya
zao hilo na mawe na mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito wakati wa
mavuno.
“Katika kukabiliana na changamoto
hizo, Serikali imeboresha mfumo wa uuzaji wa korosho kwa kuimarisha
usimamaizi na ukaguzi kuanzia ngazi ya vyama vya msingi, maghala makuu,
maghala aya hifadhi na kutoa elimu, kurejesha kwa kiwanda cha BUCCO cha
mkoani Lindi cha ubanguaji wa korosho, ujenzi wa maghala matatu ya
kuhifadhia korosho katika mikoa ya Lindi, Pwani na Tanga ili kuongeza
kiwango cha uhifadhi na ubora wa korosho pamoja na kuzalisha miche bora
10,000,000 na kuisambaza kwa wakulima bure,”alisema Mgumba.
Naibu Waziri Mgumba ameongeza
kuwa mikakati mingine ni pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani katika
zao la korosho ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usambazaji wa
pembejeo za kilimo kwa wakati, kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka
mazingira wezeshi na kuwajengea uwezo wabanguaji wa ndani kwa lengo la
kuongeza thamani ya korosho inayozalishwa nchini.
Akijibu swali la nyongeza kutoka
kwa Mbunge wa Mtama, Mhe. Nape Nnauye aliyetaka kujua hatua
zilichukuliwa na Serikali kuhusu vitendo vya rushwa katika kuhakiki
ununuzi wa Korosho, Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga alisema kuwa
wote waliojihusisha na vitendo hivyo hatua kali zilichukuliwa dhidi yao
ikiwemo kusimamishwa kazi.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa
na dhamira ya dhati ya kuwainua wakulima nchini ikiwemo wa korosho kwa
kuongeza bei ya korosho na kusimamia ununuzi wake. Jambo ambalo limekuwa
kichocheo kwa wakulima wengi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na
Tanga kujikita katika kilimo hicho.
Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Magufuli mwishoni mwaka 2018 alisema Serikali itanunua korosho kwa bei
ya shilingi 3,300 kwa kilo. Jambo ambalo lilifanyiwa kazi na wakulima wa
zao hilo wanafurahia bei hiyo na kutambua kuwa Serikali inawajali.
No comments :
Post a Comment