Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Soni wilayani Lushoto akiwa katika
ziara ya mkoa wa Tanga, Novemba 1, 2018
……………………
*Aagiza vijiji vyenye shida ya maji Bumbuli vibainishwe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali itahakikisha wananchi katika vijiji vyote nchini
wanapata huduma ya safi na salama wakiwemo na wa jimbo la Bumbuli.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza
Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto, Charles
Boy afanye utafiti na kubainisha vijiji vyenye shida ya maji Bumbuli.
Amesema baada ya kuvibaini vijiji
hivyo, anatakiwa aweke mpango wa kuhakikisha navyo
vinapata huduma ya
maji safi ili kuwaondolea wananchi tatizo hilo la ukosefu wa maji.
Alitoa agizo hilo jana jioni
(Alhamisi, Novemba 1, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mponde jimbo la Bumbuli,
Lushoto.
Waziri Mkuu ambaye jana
alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga,
aliwapongeza wakazi wa wilaya ya Lushoto kwa kutunza mazingira na vyanzo
vya maji.
Alisema Serikali ya Awamu ya
Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa
maji safi na salama katika maeneo yote yenye changamoto hiyo nchini.
“Serikali kupitia Kampeni ya Rais
Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi
katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama.”
Waziri Mkuu aliongeza
kuwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa
vipaumbele vya Serikali, hivyo aliwataka wananchi waendelee kuiamini
Serikali yao.
Awali,Naibu Waziri wa Maji, Jumaa
Aweso alisema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi,
ukarabati wa miradi ya maji, ambapo mkoa wa Tanga umetengewa sh. bilioni
13.
Aweso alitumia fursa hiyo kutoa
rai kwa wakandarasi wanajenga miradi ya maji wazingatie viwango vya
ubora kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika kugharamia miradi
hiyo.
“Serikali inatoa fedha kwa ajili
ya miradi ya maji alafu mnazitumia kujengea majumba na kununua magari,
safari hii mtazitapika tunataka miradi itekelezwe kwa kuzingatia
viwango.”
Waziri huyo aliahidi kufuatilia
kwa kina ujenzi wa miradi yote ya maji nchini ili kuhakikisha kama
inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa katika miradi hiyo.
No comments :
Post a Comment