Friday, November 2, 2018

PSSSF yaanza kulipa madeni yaliyokuwa wastaafu wa PSPF


MMGL0274.jpgMeneja Kiongozi Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa PSSSF, Eunice Chiume. Picha ya maktaba yetu.

Na Christian Gaya: Ijumaa, 2 Novemba 2018: www.majira.co.tz
KATIKA mkakati wa kuboresha huduma na kupunguza matumizi katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini, Serikali iliamua kuunganisha  Mifuko minne ya PSPF, PPF, GEPF  na LAPF na kuunda Mfuko mmoja unaojulikana kama Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa ...
Umma (PSSSF).
Aidha ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ufanisi zaidi na kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii, Serikali pia iliamua Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii NSSF uendelee na jukumu la kuhudumia wafanyakazi wa Sekta Binafsi na Sekta Isiyo rasmi tu.
Hivyo basi, Meneja Kiongozi Mkuu wa Uhusiano na Masoko wa mfuko wa PSSSF  Eunice Chiume, anasema wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa tayari wamehamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao sasa zinaendelea kutolewa na mfuko huo.
“Hii imejumuishwa pamoja na rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa nayo tayari imeshahamishiwa kwenye mfuko huu mpya wa PSSSF” Chiume anaongezea.  
Anasema baada ya kutangazwa kuanza kwa Mfuko wa PSSSF, pamoja na mambo mengine uongozi mpya ulikuwa na jukumu la kwanza la kulipa madeni ya malipo ya mkupuo kwa wanachama wa waliokuwa wa mfuko wa pensheni wa PSPF.
Chiume anasema idadi yao ilikuwa ni wastaafu wapatao 7,924 wenye jumla ya Sh. bilioni 738.43 za Kitanzania. Na mpango huu wa kulipa madeni haya uliidhinishwa na Bodi ya PSSSF kwa kuzingatia mtiririko wa kifedha kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia Agosti 2018.
Anasema kwa Agosti 2018 tu Mfuko wa PSSSF uliwalipa wastaafu  wapatao 896 hawa wakiwa ni wa Julai 2017 tu, ambapo kati hao 755 wakiwa wa fao la kustaafu na wapatao 141 wakiwa wanufaika wa fao la urithi na hivyo basi Mfuko ulitumia jumla ya Sh.65,381,743,855.48 kwa wastaafu wote. Hii ikiwa ni mara tu Serikali ilipotangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma (PSSSF) Agosti1.
“Orodha iliyohakikiwa na Hazina na kupitishwa kwa ajili ya malipo ina wastaafu wa umri wapatao 5,904. Kati ya hao hundi zipatazo 1,123 zenye jumla ya Sh. 94,484,375,322.57 zikiwa ni zile zilizotakiwa kulipwa kati ya mwezi Agosti mpaka Novemba 2017 zilitolewa kwa malipo kati ya Oktoba 5 na Oktoba mwaka huu.    Ambapo kati ya Wastaafu wapatao 814 wa mwezi Desemba 2017 wanategemewa kulipwa mwishoni mwezi huu wa Oktoba 2018,” Chiume anafafanua.
Anasema kwa Novemba 2018 watalipwa wastaafu wapatao 1,603 hawa wakiwa ni wale wa mwezi Januari – Machi 2018. Wakati kwa Disemba 2018 wamepagwa kulipwa wastaafu 931, wakati wa Aprili - Mei 2018 na waliobaki 1,372 watalipwa Januari 2019.
Anasema wastaafu wapatao 1,292, Hazina ilishauri wafanyiwe kwanza uhakiki zaidi kabla ya kuanza kulipwa pensheni zao, ambapo kati yao wapo waliondoka kazini kwa kufukuzwa, kuacha kazi, kuwa na umri zaidi ya miaka 60, vyeti feki na marekebisho ya muundo.
Malipo ya wastaafu walioingia kwenye Mfuko mpya wa PSSSF kuanzia tarehe mosi Agosti 2018 na kuendelea, wao wanaendelea kulipwa, ambapo hadi sasa madai yapatayo 326 yameshalipwa tayari. “Lengo Letu ni kuendelea kuwalipa ndani ya muda unaotajwa kisheria hadi madai ya nyuma yatakapokamilika na baada ya hapo watalipwa mapema zaidi.” Alifafanua zaidi.
Anasema wakati madai ya kipindi kabla ya kuanza kwa Mfuko wa PSSSF ambayo hayakuwa yamelipwa na mifuko kutokana na sababu mbalimbali yameletwa makao makuu kwa ajili ya kukamilishwa na kuandaliwa malipo.  Madai hayo ni jumla ya 3,876 yakijumuisha madai ya mafao ya uzazi, malipo ya mfumo wa hiari, kujitoa na kupunguzwa kazi. “Madai hayo sasa yameletwa hapa PSSSF makao makuu Dodoma kwa uchambuzi na malipo kwa madai yanayostahili,” Chiume anaeleza
Wakati huo huo, Chiume anasema mifumo mikuu mitatu ya kielektoniki tayari imeshaandaliwa na iko katika hatua za mafunzo kwa watumiaji mikoani baada ya kuwa imehakikiwa makao makuu.
“Mifumo hii ni mfumo wa kutunza kumbukumbu za wanachama yaani SSIP, mfumo wa mishahara ya watumishi na mfumo wa fedha yaani Navision Dynamics.  Mifumo mingine kama vile barua pepe za watumishi wa Mfuko na tovuti, iko tayari. Tovuti itakuwa hewani muda si mrefu baada ya kuwekewa taarifa zote muhimu.
Anafafanua ya kuwa ofisi zimefunguliwa nchi nzima na tayari watumishi wamehamishiwa. Kazi inayoendelea kufanyika ni kuunganisha mifumo iliyotajwa hapo kwenye ofisi hizo kuhamisha samani na vitendea kazi pamoja na kuzifanyia kuwekewa alama za Mfuko wa PSSSF yaani branding.
Kwa upande wa uhamisho wa watumishi, anasema tayari watumishi wa Mifuko yote yaani wa kutoka LAPF, PPF, PSPF, na GEPF wamesha pangiwa vituo na kuhama, tayari kwa ajili ya kutoa huduma vituoni mwao.
Wakati kwa upande wa kufunga hesabu za mifuko, Eunice anaeleza ya kuwa hesabu za mifuko iliyoungana zimeshafungwa na sasa kazi ya ukaguzi inakamilishwa tayari. “Hesabu hizo zitajumuishwa kuwa hesabu za mwanzo za Mfuko wa PSSSF. Kazi hii ya kuunganisha inategemewa kukamilika mwezi Desemba 2018,” Chiume  anafafanua zaidi.
Kwa upande wa taarifa kwa waajiri, anasema waajiri wanaendelea kutembelewa na kupewa taarifa juu ya kuunganishwa kwa mifuko na utaratibu wa kuwasilisha michango. Pamoja na haya yote, hata akaunti mpya za mfuko zimeshafunguliwa tayari kila mkoa kwa ajili ya kupokelea michango kutoka kwa waajiri wote nchini.

No comments :

Post a Comment