Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimuuliza maswali mwanafunzi wa VETA
Moshi, Jesca Jonathan (mwenye rasta), kuhusu utaalamu wa kuchonga vito na
madini alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji,
yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Wa
pili kulia ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
NA OWM, GEITA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wachimbaji wadogo wa madini waende Benki wakakope mitaji kwa sababu
wana uhakika wa kudhaminiwa na Benki Kuu.
“Msihofu kukopa, kukopa ni jambo la
kawaida sana. Nenda mkakope ili mpate mitaji ya kununua mitambo ya kuchenjua dhahabu
na madini mengine,” amesema.
Ametoa wito leo (Jumapili, Septemba 30,
2018) wakati akifunga maonesho ya mkoa wa Geita ya dhahabu, madini, teknolojia
ya madni na uwekezaji yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini
Geita. Maonesho hayo yalianza Septemba 24, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema, wakati akikagua
mabanda ya maonesho kwenye viwanja hivyo, ameelezwa kwamba gharama ya mtambo
unaohitajika kwa wachimbaji wa kati inafikia sh. milioni 10. “Naomba niwaeleze
wanaGeita kwamba mnakopesheka, nendeni mkaombe mikopo ili mnunue mitambo ya
kuchenjua dhahabu,” amesisitiza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaeleza wana-Geita
kwamba siri kubwa ya kufanikiwa kupata mikopo ni kwa wao kuunganisha nguvu kwa
kujiunga kwenye vikundi ili wawe na malighafi ya kutosha mitambo hiyo.
“Wakuu wa wilaya za Mkoa huu simamieni
zoezi hili kwa sababu wilaya zenu zote zinachimba madini. Simamieni uundaji wa
vikundi na mwende mkawasemee benki pale wanapokwama.”
Akielezea kuhusu makusanyo ya fedha kutokana
na mauzo ya dhahabu kwenye mkoa huo, Waziri Mkuu amesema tangu Aprili mwaka
huu, mapato yanayotokana na madini yameongezeka kutoka sh. milioni 400 na
kufikia sh. milioni 850 Agosti, mwaka huu.
Katika hatua
nyingine, Waziri
Mkuu amewataka wazazi wawapeleke watoto wao kwenye vyuo vya ufundi vya VETA ili
wakajifunze taaluma ya uchongaji wa madini na vito kama eneo jipya la ajira
nchini.
“Nimemuona binti mmojakwenye banda la
VETA akielezea vizuri kuhusu uchongaji wa madini na vito. Nikabaini kumbe jambo
hili linaweza kufanyika hapa nchini kwetu. Ninawasihi Wazazi pelekeni watoto
wenu kwenye vyuo vya VETA vya Mwanza, Geita na Moshi ambako kozi hii inafundishwa,”
amesisitiza.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria maonesho hayo, Waziri wa Madini, Bibi
Angella Kairuki alisema sekta ya madini ilichangia pato la Taifa kwa asilimia
4.8 tu, licha ya kuwa sekta hiyo iliongoza kwa kuingiza fedha za kigeni
kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya nchi katika mwaka 2016/2017.
Alisema lengo la Serikali ni
kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka
2025.
Alisema zaidi ya asilimia 90 ya thamani
ya madini yanayouzwa nje ya nchi ni dhahabu na kwamba mkoa wa Geita unaongoza
kwa uzalishaji wa dhahabu ambapo katika mwaka 2017, asilimia 41.2 ya dhahabu
iliyouzwa ilitoka kwenye mkoa huo.
“Kwa upande wa wachimbaji wadogo
wanaozalisha dhahabu, mkoa wa Geita unaongoza ambapo tani 1.175 za dhahabu
zenye thamani ya shilingi bilioni 89 zilizalishwa, na kati ya hizo, asilimia 49
ilizalishwa na wachimbaji wadogo,” alisema.
Alisema takwimu hizo zilipatikana kabla
Serikali haijachukua hatua ya kuzuia usafirishaji wa carbon yenye dhahabu kuvuka mipaka ya mkoa, hali iliyokuwa
inachangia utoroshaji, ukwepaji wa kodi na jamii husika kushindwa kunufaika na
madini yayiyopo kwenye maeneo yao.
Maonesho hayo yamekutanisha makampuni
250 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na yataendelea hadi Jumatano jioni,
Oktoba 3, 2018 kutokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert
Gabriel kwa Waziri Mkuu ili wananchi wa mkoa wake wapate fursa zaidi ya
kujifunza masuala ya madini, uwekezaji na matumizi ya teknolojia sahihi
zinazozingatia utunzaji wa mazingira.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ambayo
ni ya kwanza kufanyika nchini, inasema: “Teknolojia
bora ya uzalishaji dhahabu kwa maendeleo ya kijamii na uchumi wa viwanda”.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kifungashio cha kopo la kahawa
aina ya AMIMZA alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya dhahabu, madini,
teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika kwenye viwanja vya
Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Kulia ni Afisa mauzo wa TANICA
PLC, Revina Peter akitoa maelezo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea maelezo ya mtambo wa kuchenjua
madini unaoweza kumilikiwa na wachimbaji wa kati alipotembelea mabanda kwenye
maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika
kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Anayetoa
maelezo ni Katibu Msaidizi wa UMUMAGE, John Ngenda.
Mwanafunzi wa mwaka pili katika chuo cha VETA Moshi, Careen Vedasto
akiendesha kifaa cha kuchimbia madini kilichobuniwa na wanafunzi na walimu wa
chuo hicho mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya
dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika kwenye
viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Mhandisi Robert Gabriel.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Mhandisi Robert Gabriel, mara baada ya kuwasili mkoani humo kufunga maonesho ya
dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji yaliyofanyika kwenye viwanja
vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018.(PICHA NA OWM)
No comments :
Post a Comment