Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa,
Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa
Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye
uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani utakaofanyika katika jimbo la Liwale
na kwenye kata 37 leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia
akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi
na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi
mdogo wa Ubunge na udiwani utakaofanyika katika jimbo la Liwale na
kwenye kata 37.
Mkurugenzi wa
Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel
Kawishe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria wakati wa
mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa
Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Oktoba
13 mwaka huu.
Wajumbe wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji
wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) wakifuatilia mada
mbalimbali wakati wa Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo, jijini
Dodoma.
Wajumbe wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji
wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) wakiwa katika
picha ya
pamoja na baadhi washiriki wa Mafunzo kwa Wasimamizi wa
Uchaguzi Mdogo, jijini Dodoma leo.
Wasimamizi wa
Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Oktoba 13 mwaka huu
katika jimbo la Liwale na kwenye Kata 37 za Tanzania Bara wametakiwa
kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na
Kanuni za uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim
Mbarouk ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya
siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi
kutoka katika maeneo yenye uchaguzi.
Jaji Mbarouk
amewataka Wasimamizi hao kufanya kazi kwa ufanisi, uhuru, uwazi na bila
kuegemea upande wowote ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.
Amesema uchaguzi
ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa
kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo
msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.
“ Tunakutana hapa
ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha
zoezi la uchaguzi lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto
mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,
natumaini mtatumia fursa hii kubadilishana uzoefu katika kutekeleza
jukumu hili lililo mbele yenu” Amesema Jaji Mbarouk.
Jaji Mbarouk
ametoa wito Wasimamizi hao waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa
Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi akisisitiza kwamba katika kipindi
hiki chaguzi zinafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya
Kisiasa, kutoaminiana na wakati mwingine kutawaliwa na mihemko ambayo
imekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Aidha, amewaeleza
Wasimamizi hao kuwa wameaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo kwa
kuwa wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi hivyo wajiamini na kujitambua.
Ametoa wito kwa
Wasimamizi hao kuhakikisha kwamba wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi na
wanawatumia vyema wasaidizi walio nao katika maeneo yao ya kazi kwa
matokeo bora.
“Naomba mjue mna
jukumu la kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wote wa uchaguzi
kwa Tume. Hivyo mfanye kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, bila kuegemea
upande wowote.Kufanya kazi kwa uhuru na kwa uwazi kutasaidia kudumisha
amani katika maeneo yenu ya Uchaguzi” Amesema.
Kuhusu kufanyika
kwa Uchaguzi huo mdogo Oktoba 13 mwaka huu, Jaji Mbarouk amesema kuwa
kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi, Sura 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya
Serikali za Mitaa, Sura 292, ni jukumu la Tume kusimamia, kuendesha na
kuratibu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi.
Amesema kwa
nyakati tofauti Tume imepokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia Kifungu cha 37 (3)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 aliitaarifu Tume uwepo wa
nafasi wazi za Ubunge katika jimbo la Liwale.
Pia amefafanua
kuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia
masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya
Mitaa, Sura, 292 alitoa taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani
katika Kata 37 kutoka katika Halmashauri 27 zilizopo katika Mikoa 13 ya
Tanzania Bara.
Katika hatua
nyingine Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mbarouk Salim Mbarouk ameeleza
kuwa jumla ya wagombea 6 waliteuliwa kugombea ubunge katika jimbo la
liwale ambapo mgombea mmoja alijitoa baada ya uteuzi huo kukamilika.
Ameongeza kuwa katika Kata 37 za Tanzania Bara jumla ya wagombea 56 waliteuliwa kugombea udiwani katika Kata hizo.
No comments :
Post a Comment