Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasili Ofisi Kuu ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga kwa ajili ya kuzungumza na
wafanyakazi wa Mamlaka hiyo.
Meneja wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania mkoa wa Tanga, Bw. Masawa Masawa, akiwasilisha
taarifa ya Mamlaka hiyo ambapo alimweleza Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kuhusu mafanikio na changamoto
zinazoikabili TRA mkoani mwake katika kutimiza majukumu ya kukusanya
kodi ambapo wastani wa ukusanyaji kodi katika kipindi cha miaka minne
uko asilimia 80.
Meneja wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania mkoa wa Tanga, Bw. Masawa Masawa, akiwasilisha
taarifa ya Mamlaka hiyo ambapo alimweleza Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kuhusu mafanikio na changamoto
zinazoikabili TRA mkoani mwake katika kutimiza majukumu ya kukusanya
kodi ambapo wastani wa ukusanyaji kodi katika kipindi cha miaka minne
uko asilimia 80.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisisitiza masuala ya
ubunifu na uadilifu kwa wafanyakazi wa TRA nchi nzima ili kuongeza
mapato ya Serikali kwa njia ya kodi bila kuwabughudhi walipa kodi na
kukemea vitendo vya rushwa, alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi wa
TRA, Jijini Tanga. Kulia kwake ni Meneja wa TRA mkoani Tanga, Bw. Masawa
Masawa.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (mbele), akizungumza na
wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoani Tanga na
kusisitiza umuhimu wa kudhibiti biashara ya magendo katika mwambao wa
Tanga ili kuongeza mapato ya Serikali.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (aliyeketi kulia), akiwa
katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) mkoa wa Tanga, baada ya kumalizika kwa mkutano wake na wafanyakazi
hao, Jijini Tanga.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiagana na wafanyakazi
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tanga, baada ya kumalizika
kwa mkutano wake na wafanyakazi hao, Jijini Tanga.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Tanga
Waziri wa Fedha
na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania TRA, kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu
wafanyakazi wake wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili
ikiwemo rushwa na kutumia njia zisizokubalika wakati wa kukusanya kodi
za Serikali.
Dkt. Mpango
ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRA Mkoa wa
Tanga, ambapo ameagiza wafanyakazi wawili wa mamlaka hiyo, Robinson
Munisi na Abraham Maleko waondolewe kwenye kazi wanazofanya sasa na
kupangiwa kazi nyingine baada ya kuwepo kwa tuhuma za ulevi wa
kupindukia na kujihusisha na mtandao wa wafanyabiashara unaotumika
kuikosesha Serikali mapato yake
Amewataka
watumishi wa mamlaka hiyo kuwa waadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya
rushwa na lugha za kuudhi kwa wateja wao ili kupunguza malalamiko kutoka
kwa walipa kodi na kuonya kuwa serikali haitomvumilia mtumishi yeyote
atakayefanya kazi kinyume na maadili ili kujenga nidhamu kwa watumishi
hao na hatimaye kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
“Mwambieni
Kamishna Mkuu wa TRA (Bw. Charles Kichere) kwa watumishi hawa siwataki,
wapelekeni maeneo mengine mbali huko na muendelee kuwachunguza, na
nataka kupata taarifa ya watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya
utumishi wa umma ikiwemo kujihusisha na rushwa” alisisitiza Dkt. Mpango
Aidha, amemwagiza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Kamishna
Mkuu wa TRA, Bw. Charles Kichere, kuhakikisha boti la doria katika
Mwambao wa Bahari mkoani Tanga linapatikana haraka ili kuzuia biashara
ya magendo inayoyofanywa kwa kutumia bandari bubu hivyo kuikosesha
Serikali mapato yake.
“Ni lazima jambo
hili lifanyike haraka kwa sababu ya umuhimu wake kwasababu si tu kwamba
Serikali inapoteza mapato yake kutokana na vitendo hivyo vya kuvusha
magendo kupitia bandari bubu lakini pia ni hatari kwa usalama wa Taifa
kwa sababu maadui wanaweza kupitisha silaha” alionya Dkt. Mpango.
Akisoma taarifa
fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Mamalaka hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa
Tanga Bw. Masawa Masawa alisema makusanyo ya Mkoa huo yamekuwa
yakiongezeka Mwaka hadi Mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka
2013 hadi 2017 ambapo katika Mwaka 2016/17 Mkoa ulikusanya Shilingi
bilioni 107.39 kati ya Shilingi bilioni 131.06 ya malengo kwa Mwaka huo
ambayo ni sawa asilimia 82 ya makusanyo.
Kuhusu maadili ya
wafanyakazi wa Mamlaka hiyo mkoani Tanga, Bw. Masawa amesema kuwa
pamoja na kuwapa elimu kuhusu maadili mema kupitia Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa TAKUKURU, wamekuwa wakiwachukulia hatua kali
watumishi wao wanaobainika kujihusisha na vitendo vinavyochafua taswira
ya mamlaka hiyo.
Akihitimisha
mkutano huo, Dkt. Mpango, alimwagiza Meneja huyo kupandisha kiwango cha
ukusanyaji mapato kwa asilimia 100 na kutoa onyo kwa Mameneja wote wa
TRA nchini watakaoshindwa kufikia lengo hilo wajitathmini kama wanatosha
kwenye nafasi zao.
No comments :
Post a Comment