Friday, June 29, 2018

Askofu mwenye watoto 149 afungwa, ana wake 24


Viongozi wawili wa dini, mmoja akiwa askofu nchini Canada wamehukumiwa kifungo cha ndani (house arrest) pamoja na kipindi cha matazamio, kwa kosa la kuoa wanawake wengi na kuzaa watoto wengi. Shirika la habari la AP, limeripoti kuwa [Askofu] Winston Blackmore na mwenzake James Oler walikutwa na hatia mahakamani tangu Julai mwaka jana lakini wiki hii wamehukumiwa.
Blackmore ana wanawake 24 pamoja na watoto 149 huku Oler akiwa na wanawake watano.
Mahakama imemhukumu Blackmore mwenye umri wa miaka 61, kifungo cha ndani ya nyumba kwa miezi sita pamoja na mwaka mmoja wa kipindi cha uangalizi/matazamio (probation). Wakati huohuo, Oler mwenye umri wa miaka 53 amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu cha ndani ya nyumba pamoja na mwaka mmoja wa uangalizi/matazamio.

Mbali na hukumu hiyo, Mahakama hiyo imempa adhabu Blackmore ya kufanya kazi za kijamii kwa saa 150 pamoja na Oler saa 75. Awali, wawili hao walikuwa wanakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela.
Gazeti la nchini humo la Globla News, limeripoti kuwa Blackmore alianza kuwaoa wake zake tangu miaka zaidi ya ishirini iliyopita. Imeelezwa kuwa alipokuwa anawaoa wanawake hao, wanawake 10 aliwaoa wakiwa na umri wa miaka 17, watatu walikuwa na umri wa miaka 16 na mmoja alikuwa na umri wa miaka 15.

Walikuwa wakifanya kazi kama maaskofu wa kanisa linalofahamika kama ‘Fundamentalist Church of Jesus Christ of Latter-Day Saints’
Wawili hao wamekuwa watu wa kwanza kukutwa na hatia ya kushiriki ndoa za mitala tang mwaka 1906, kwa mujibu wa CBC.
Kesi yao ilivuta hisia za watu wengi na kuzua mijadala kwani sheria ya kudhibiti ndoa za mitala ilikuwa na upinzani mkubwa.
Mahakama Kuu ilibariki rasmi matumizi ya sheria hiyo mwaka 2011 na kutoa mwanya kwa washtakiwa kuanza kufikishwa mahakamani.
Mawakili waliokuwa wanawatetea hawakutaka kuzungumza na waandishi wa habari.

No comments :

Post a Comment