WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza kaulimbiu yake ya kujenga
uchumi unaotegemea viwanda na kwamba hadi kufikia Februari 2018, viwanda
vipya 3,306 vimekwishaanzishwa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano,
Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya
mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na
mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa 11 wa
Bunge.
Amesema Serikali inahamasisha
uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi
kwa wawekezaji mahiri (strategic investors); kuendeleza na kuboresha
miundombimu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji.
“Serikali itaendelea kuhuisha sera, sheria na kanuni pamoja na
kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua
stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya mauzo,” amesema.
Waziri Mkuu amelieleza Bunge
kwamba mikoa na Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya
uwekezaji kwa ajili ya viwanda na kwamba katika mwaka 2018/2019,
Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kielelezo,
uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi pamoja na kuboresha mazingira ya
biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.
Akitoa ufafanuzi kuhusu ushiriki
wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda, Waziri
Mkuu amesema pamoja na miradi mingine NSSF na PPF kwa kushirikiana na
Jeshi la Magereza wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari
mkoani Morogoro.
“Lengo la mradi huo ni kuzalisha
tani 250,000 za sukari na umeme megawati 40. Mradi huo unatekelezwa
katika shamba la Mkulazi lililopo Ngerengere lenye ukubwa wa hekta
63,000 na shamba la gereza la Mbigiri lenye ukubwa wa ekari 12,000
lililopo Dakawa,” alisema.
“Hadi sasa ekari 2,000 za
mashamba ya miwa zimetayarishwa katika eneo la Mkulazi na ekari 1,100
zimepandwa miwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha awamu ya kwanza ya
ufungaji wa mitambo ya kiwanda cha Mbigiri ifikapo mwezi Desemba, 2018
ili uzalishaji uanze mwaka 2019,” alisema na kuongeza kuwa miradi hiyo
itakapokamilika, itazalisha zaidi ya ajira 100,000.
Waziri Mkuu alisema tangu kuanza
kwa utekelezaji wa mradi huo Juni 2017, ajira za moja kwa moja 780 na
ajira zisizo za moja kwa moja 24,000 ikijumuisha wakulima wadogo wa
mbegu na kilimo cha nje zimezalishwa.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa
barabara kuu, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kuboresha mtandao
wa barabara nchini ambapo katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari
2018, ujenzi wa Km. 776.45 za barabara kuu kwa kiwango cha lami
umekamilika na Km. 1,760 zinaendelea kujengwa. Pia barabara zenye urefu
wa Km. 17,054 zilikarabatiwa katika kipindi hicho.
Kuhusu ujenzi wa madaraja, Waziri
Mkuu alisema madaraja ya Kilombero na Kavuu ujenzi wake umekamilika na
kwamba ujenzi unaoendelea hivi sasa ni wa madaraja ya Sibiti, Mto Mara,
Lukuledi, Ruhuhu, Momba na Mlalakuwa. Alisema madaraja mengine 996
katika maeneo mbalimbali nchini yamekarabatiwa.
Kuhusu jitihada za Serikali
kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu
alisema hadi kufikia Februari 2018, ujenzi wa barabara ya juu katika
eneo la TAZARA ulikuwa umefikia asilimia 70 na ujenzi wa barabara za juu
katika makutano ya Ubungo (Ubungo Interchange) umeanza.
“Maandalizi ya awamu ya pili hadi
ya nne ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka
yanaendelea. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kujenga kilometa
597 za barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami na kilometa 72 za
kiwango cha lami zitakarabatiwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuliarifu Bunge juu ya uanzishwaji wa Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency –
TARURA) kwa lengo la kurahisisha huduma za usafirishaji na kuongeza
kasi ya wananchi kujiletea maendeleo.
Alisema TARURA imepewa jukumu la
kusimamia ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara zenye urefu wa
kilometa 108,946.2 za vijijini na mijini. “Katika mwaka 2017/2018,
TARURA imesimamia matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita
4,183.3, madaraja 35, makalavati makubwa 43 na madogo 364 na drift nne,” alisema.
Waziri Mkuu aliliomba Bunge
likubali kupitisha sh. 143,618,762,698 zikiwa ni makadirio ya mapato na
matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizopo chini yake
pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019 ambapo sh. 74,527,321,698
ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 69,091,441,000 ni kwa ajili
ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Waziri Mkuu aliliomba
Bunge liidhinishe sh. 125,521,100,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo
sh. 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
8,315,613,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
No comments :
Post a Comment