Na Jumia Travel Tanzania
Miongoni mwa mikoa maarufu nchini
Tanzania ni pamoja na Tanga. Ukiachana na ukaribu wake na jiji la Dar es
Salaam, mkoa wa Tanga una utajiri wa utamaduni wa Waswahili
wanaopatikana katika pwani ya bahari ya Hindi, makumbusho ya kihistoria,
shughuli za uchumi na kibiashara, pamoja na wanasiasa na wanasanaa
mbalimbali mashuhuri wanaolipeperusha vema jina la mkoa huu.
Hivi karibuni mkoa wa Tanga umekuwa ni
eneo mojawapo la kitalii linalokua kwa kasi na kuwavutia watalii wengi
ndani na nje ya Tanzania. Watalii wengi kupendelea kwenda Tanga kunaweza
kusababishwa na sababu kadhaa zikiwemo miongoni mwao tayari
wamekwishatembelea sehemu zingine, kupata simulizi kutoka kwa watu wao
wa karibu pamoja na vivutio vingine ambavyo havipatikani sehemu zingine
isipokuwa Tanga.
Jumia Travel imekukusanyia baadhi ya sababu ambazo zimepelekea watu wengi kupendelea kwenda kutalii mkoa wa Tanga:
Jiografia. Asilimia kubwa ya watalii
hupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo katika
jiji la Dar es Salaam. Umbali uliopo kati ya jiji hili na mkoa wa Tanga
sio mkubwa, huchukua muda wa takribani masaa 6 kitu ambacho watalii
wengi huweza kumudu. Hii imerahisisha shughuli za kitalii kwa urahisi
kwa sababu watalii wanaweza kwenda na kurudi kwa urahisi.
Hali ya hewa. Miongoni mwa mji mashuhuri
kwa shughuli za kitalii hivi sasa mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla
ni Lushoto. Hali ya hewa nzuri, mandhari ya kuvutia na hoteli za kitalii
katika eneo hili zimekuwa ni hamasa kubwa kwa wasafiri wengi. Eneo la
Lushoto ambalo linapatikana kwenye safu ya milima ya Usambara
limejizolea umaarufu kutokana na shughuli tofauti za kitalii kama vile
matembezi na kupanda milima, shughuli za uvuvi, kuendesha baiskeli,
kutembelea makumbusho ya kale, nakadhalika. Na kwa kuongezea eneo hili
limewekezwa kwa hoteli za kisasa za kitalii.
Hoteli za kitalii. Kutokana na kuwepo
kwa shughuli nyingi za kitalii, kumekuwa na uwekezaji mkubwa katika
huduma ya malazi. Miongoni mwa changamoto kubwa inayoikumba sekta ya
utalii nchini na duniani kote ni huduma ya malazi. Malazi ni huduma
ambayo huwa ghali ukilinganisha na huduma nyingine kama vile usafiri wa
kwenda na kurudi, viingilio na makato mengineyo.
Mkoa wa Tanga umejitahidi kwa hilo,
wafanyabiashara wengi wamejenga hoteli ili kuweza kukidhi haja ya kila
aina ya mtalii. Si jambo la kushangaza kukuta hoteli za kitalii karibu
na vivutio vya kitalii.
Gharama nafuu. Miundombinu kama vile
barabara imewavutia watu wengi kwenda kwa urahisi kutalii vivutio vya
mkoa wa Tanga kwani imerahisisha gharama za usafiri. Ukiachana na
usafiri wa mabasi yanayokwenda na kurudi kila siku, watu wengi siku za
hivi karibuni wamekuwa wakitumia usafiri wao binafsi. Unafuu pia upo
kwenye huduma ya malazi ambayo kila mtu anaweza kumudu pamoja na gharama
za kuishi kwenye jiji hilo kwa ujumla.
Ukarimu wa watu wake. Watu wa Tanga
wanasifika kuwa na haiba ya ukarimu kama walivyo watanzania wengi
nchini. Hiki nacho kimekuwa ni kivutio kingine kwa watalii wengi
kutembelea eneo hilo. Ukarimu huwavuta watalii wengi, kuwajengea hali ya
usalama na kujifunza mengi kutoka kwa wenyeji wao. Wakazi wa Tanga
wanatoa mchango mkubwa katika kulitangaza jiji lao kitalii kwa kuwapokea
wageni na kuwafunza mambo yanayopatikana mkoani mwao.
Kama ulikuwa unafikiria sehemu ya kwenda
kutalii tofauti na sehemu ulizozizoea, Tanga itakuwa ni chaguo sahihi
kwa hivi sasa. Ni miongoni mwa sehemu zinazofikika kwa urahisi na
unaweza kufanya shughuli nyingi ndani ya muda mfupi na kurejea kwenye
majukumu yako ya kawaida.









No comments :
Post a Comment