Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba
Kabudi akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria
uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, kushoto ni Katibu Mtendaji wa
Tume Casmir Kyuki na kulia ni Katibu wa Baraza Ambokile Mwakasungula.
NA
MUNIR SHEMWETA, MOROGORO
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesisitiza umuhimu wa
kuwashirikisha watumishi katika mipango ya uendeshaji Taasisi kwa kuwa suala hilo
lipo kisheria.
Aidha,
alisema kwa miaka yote Serikali imekuwa ikisisitiza Taasisi kujenga na
kutekeleza utaratibu wa kushirikisha watumishi na hali hiyo inatokana na ukweli
kuwa palipo na watumishi wengi pana mawazo mengi.
Profesa
Kabudi alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano wa kumi na tatu
wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania uliofanyika
katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.
‘’Ushirikishwaji
watumishi kwenye mipango ya uendeshaji ofisi unasaidia kupata mawazo mengi na
mapya yanayoweza kurahisisha uendeshaji wa ofisi na kutoa fursa ya kusikiliza
kero na changamoto kwenye uendeshaji wa Taasisi na kushirikiana katika kutafuta
ufumbuzi’’ alisema profesa Kabudi.
Aliongeza
kuwa, kwa kushirikiana na watumishi ni dhahiri wanapata morari wa kushiriki
kikamilifu kwenye utekelezaji wa mipango ya taasisi ambayo wao wenyewe
walishiriki kuiandaa.
Waziri
huyo wa Katiba na Sheria alisema, ushirikishwaji unafanywa kupitia baraza la
wafanyakazi kwa kuwa baraza ni chombo
kinachowashirikisha wafanyakazi katika kupanga , kusimamia na kutekeleza mipango mbalimbali inayohusu shughuli za kazi za Taasisi
kama zilivyoainishwa katika sheria za nchi.
Kwa
mujibu wa Profesa Kabudi, Mabaraza hutoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki katika
maamuzi mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya wafanyakazi na uongozi pamoja na mazingira ya utendaji hasa mahala pa kazi hivyo baraza ni chombo
cha kuimarisha na kuboresha demokrasia mahala pa kazi.
Amewataka
wajumbe wa baraza wa Tume ya Kurekebisha Sheria kuzingatia suala la nidhamu
kazini, misingi ya kazi na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni,
taratibu. Aidha, alitaka uzembe kazini upigwe vita na suala la kufanya kazi kwa
mazoea kukomeshwe na kubainisha kuwa,vipaumbele viwekwe katika kulinda
rasilimali za Tume na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha na mali zake.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria
ambaye ni Katibu Mtendaji Tume Casmir Kyuki alisema katika kipindi cha Julai
2017 hadi Machi 2018 Tume yake imeweza kutekeleza majukumu yake kama
yalivyoainishwa katika bajeti.
Ameyataja
majukumu hayo kuwa ni kufanya mapitio ya Mfumo wa Sheria Unaosimamia Haki
Jinai, Sheria ya Ushahidi, Uchambuzi wa Kesi za Mahakama ya Rufaa, Mfumo wa
Sheria Unaosimamia Huduma ya Ustawi wa Jamii, Mfumo wa Sheria za Ufilisi pamoja
na kutoa elimu ya sheria kwa umma.
Ameishukuru
serikali kwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya katika sekta ya sheria kupitia
tangazo la serikali namba 48,49 na 50 ambapo yameleta muundo mpya kwa
kuanzishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai na ile ya Wakili Mkuu wa
Serikali ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria
Tanzania Casmir Kyuki (Kushoto) akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi kufungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo
Sokoine mkoani Morogoro, kulia ni Katibu wa Baraza Ambokile Mwakasungula
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba
Kabudi akimsikiliza Katibu Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Khalist
Luanda mara baada ya kufunguka mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Tume ya Kurekebisha Sheria uliofanyika katika
Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mkoani Morogoro, katikati ni Katibu Msaidizi wa
Tume (Idara ya Mapitio) Angelah Bahati
Sehemu
ya Wajumbe Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi (hayupo
pichani) wakati akifungua mkutano huo
uliofanyika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mkoani Morogoro.
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na
wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Tume ya Kurekebisha Sheria katika Chuo Kikuu
cha Kilimo Sokoine mkoani Morogoro. (PICHA
NA MUNIR SHEMWETA-TUMESHERIA)
No comments :
Post a Comment