Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
ofisini kwake Machi O2, 2018 Mjini Bariadi
……………….
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali Mkoani humo haijawakataa wadau wa
Afya kutoka katika Mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa
wanaofanya kazi mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali
kwenye Sekta ya Afya , bali inatambua mchango wao na inawaomba kufanya
kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa kwenye Sekta ya Afya.
Mtaka ameyasema hayo katika
mazungumzo maalum na waandishi wa Habari wakati alipokuwa akifafanua
kauli aliyoitoa katika kikao kilichofanyika Februari 25 na 26 Mjini
Bariadi kati ya Viongozi wa Mkoa huo na Wadau Afya mkoani humo ya
kuwataka kuelekeza zaidi fedha zao katika kujibu mahitaji ya wananchi
kwenye Afya badala ya semina na mafunzo kwa watumishi.
Amesema Serikali inatambua
mchango wa Mashirika na wadau wa Afya Mkoani humo kutokana na mambo
waliyoyafanya kuunga mkono Serikali kutatatua changamoto mbalimbali za
Sekta ya Afya, ikiwa ni pamoja na kutoa magari, kujenga majengo ya
upasuaji katika baadhi ya Vituo vya Afya na kuwajengea uwezo watumishi
wa afya.
Ameongeza kuwa pamoja na michango
hiyo Mashirika mengi yanayofanya kazi Mkoani Simiyu katika Sekta ya Afya
yameonekana kujikita zaidi katika kutoa fedha nyingi kwa ajili ya
semina na mafunzo kwa watumishi wa Afya , badala ya kusaidia katika
kutatua changamoto ambazo ni vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa pia katika
Sekta ya Afya.
Aidha. Mtaka amebainisha kuwa
Vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa katika Sekta ya Afya ni pamoja na Ujenzi
wa Miundombinu ya Afya ambayo ni majengo ya zahanati, vituo vya afya,
vyumba vya upasuaji, hospitali), Vifaa pamoja na vifaa tiba, ambapo
alieleza kuwa Mkoa huo una upungufu wa Hospitali ya Mkoa, Hospitali
mbili za Wilaya, Vituo vya Afya 112 na Zahanati 291.
“Tumepitia bajeti za mashirika
haya 11 kwa ujumla wake mwaka 2018 yatatumia zaidi ya shilingi bilioni
21, hizi ni fedha nyingi ambazo kama zitafanya kazi inayoonekana huduma
za Afya ndani ya mkoa zitaimarika, changamoto kubwa ambayo mimi kama
mkuu wa mkoa na viongozi wenzangu tumeiona ni fedha nyingi kati ya hizo
kuelekezwa kwenye mafunzo ya watumishi wa afya” alisema
“Kwanza nimeyaomba mashirika
yanayofanya kazi za Sekta ya Afya ndani ya Mkoa kila moja kuonesha kazi
wanazofanya, pili natoa wito kwa mashirika haya kuelekeza fedha nyingi
kwenye kuongeza idadi ya vituo vya afya, zahanati, vifaa na vifaa tiba
ili tunapojenga uwezo kwa watumishi wetu wa Afya wawe na mahali pa
kwenda kufanyia kazi mafunzo wanayopata” alisisitiza Mtaka
Ameongeza kuwa Ofisi yake
imeandika barua Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa ili Viongozi kutoka Wizara hizo mbili
wakutanishwe pamoja na Viongozi wa Wizara ya Afya na Viongozi wa Mkoa wa
Simiyu kwa lengo la kujadili na kuchambua tija ya fedha za
wadau/mashirika hayo kwenye Sekta ya Afya.
Mmoja wa wadau hao Mwakilishi
kutoka Shirika la Mkapa Foundation Bi.Adeline Saguti akichangia hoja
katika kikao chao na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu alisema Wadau wa Afya
Mkoani humo wameahidi kushirikiana na Mkoa huo kufanyia kazi maeneo
yenye uhitaji katika Sekta ya Afya.
Wadau wa Afya (mashirika ya ndani
na nje ya nchi) wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu ni pamoja na AMREF,
AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, Red Cross, ICAP,
TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION na BORESHA AFYA.
No comments :
Post a Comment