Meza Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti
wa Mkutano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ambaye pia ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu
kulia), kushoto kwake ni Mwenyekiti Mwenza na Mratibu wa Umoja wa
Mataifa na kiongozi wa washirika hao wa Maendeleo Bw. Alvaro Rodriguez,
mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya makazi Bi. Doroth Mwanyika (kulia) na Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Sera) Dkt. Khatibu Kazungu,
wakifuatilia kwa makini mkutano kati ya Serikali na Washirika wa
Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Mjini Dodoma.
Mwakilishi wa Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania katika mkutano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo,
Bw. Dickson Lema (kushoto) akifuatilia mjadala kati ya pande hizo mbili
uliolenga kuimarisha zaidi ushirikiano, uliofanyika mjini Dodoma.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa na
kiongozi wa washirika wa Maendeleo nchini Tanzania, Bw. Alvaro
Rodriguez, akihutubia mkutano wa kimkakati wa maendeleo kati ya Serikali
ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa St. Gasper Mjini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James akihutubia washiriki wa mkutano wa kimkakati
kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika mjini Dodoma
ukilenga kuimarisha mahusiano kati ya pande hizo mbili ili kuiwezesha
nchi kufikia malengo yake ya maendeleo.
Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara
ya Fedha na Mipango Bw. John Rubuga na Kansela Mkuu, Ushirikiano na
Maendeleo wa Canada Bi. Susan Steffen, wakifuatilia kwa makini mijadala
mbalimbali kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na
Washirika wa Maendeleo ili kufanikisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa na
Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III)), uliofanyika mjini
Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi na Somalia, Bi.
Bella Bird, nje ya ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper Mjini Dodoma,
walipokutana kujadili namna pande hizo mbili zinavyoweza kuimarisha
ushirikiano wa kimkakati zaidi ili kuharakisha maendeleo ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Shirika la
Misaada ya Maendeleo la Marekani- USAID Bw. Andy Karas, nje ya ukumbi wa
Mikutano wa St. Gasper Mjini Dodoma, walipokutana kujadili namna
Serikali na Washirika wa Maendeleo wanavyoweza kuimarisha ushirikiano wa
kimkakati zaidi ili kuiwezesha nchi kuharakisha maendeleo yake kwa
manufaa ya wananchi wake.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango
……………………
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania (SMT) imekubaliana na Washirika wa Maendeleo kurejesha
uhusiano wa karibu na wenye tija ili kusaidia kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka Mitano pamoja na
Mkakati wa
Kukuza Uchumi Zanziba (MKUZA III).
Hayo yamebainishwa mjini Dodoma na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, wakati
akifungua mkutano wa Mazungumzo ya kimkakati kama ilivyobainishwa kwenye
Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Serikali na Washirika wa
Maendeleo.
Bw. James amesema kuwa Mwongozo
huo wa miaka 7, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2014/2025,
umelenga kuipa Serikali nafasi ya kuongoza mchakato wa maendeleo na
kuijengea Serikali uwezo wa kukusanya mapato yake ya ndani, kuchambua
fursa muhimu za uwekezaji na kutumia masoko ya kikanda na kimataifa
kupata faida.
“Tumekubaliana kwamba
tutasimamia mchakato mzima wa maendeleo sisi wenyewe kama nchi, matumizi
mazuri ya rasilimali, kuimarisha uwajibikaji, kukuza biashara na
uwekezaji wa ndani na nje” alifafanua Bw. James
Amesema kuwa nchi inajivunia hatua
kubwa iliyofikiwa kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania imefikia, ikiwemo
kutambuliwa kimataifa kuwa kinara wa masuala ya ukuaji wa uchumi wa
Taifa na uchumi jumuishi, ambapo imekuwa ikifanya vizuri kimataifa,
kikanda na katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika mkutano huo
uliowashirikisha Washirika wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali duniani,
Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika hao Bw. Alvaro
Rodriguez, ameahidi kuwa watashirikiana na Tanzania ili malengo yake ya
maendeleo yaweze kufikiwa kwa kuboresha zaidi ushirikiano ambao hapo
awali ulianza kulegalega.
Ameelezea kuridhishwa na hatua
zinazochukuliwa na Serikali zote mbili-Tanzania Bara na Tanzania
Zanzibar katika kufanikisha malengo yake ya kukuza uchumi kama
ilivyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo (FYDPII) na Mkakati
wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III).
Amesema ili mipango hiyo iweze
kufanikiwa kuna umuhimu wa kuishirikisha kikamilifu Sekta Binafsi pamoja
na washirika wa maendeleo kwa kuweka mazingira ya kuongeza uzalishaji,
kukuza ajira kwa vijana wa kike na wa kiume na hatimaye kufanya
mapinduzi ya kiuchumi.
“Vijana takribani milioni moja
wanaingia katika soko la ajira kila mwaka, hivyo ni muhimu kuweka
mazingira ya upatikanaji wa ajira tena zenye staha katika kipindi hiki
ambacho nchi inafanya mapinduzi makubwa ya viwanda na uchumi”
alisisitiza Bw. Rodriguez.
Amesema kuwa uwekezaji katika
masuala ya elimu, afya, hifadhi ya jamii, kutoa fursa sawa kwa wote
(wanaume na wanawake) ni muhimu kwa kuwa jamii yenye afya itashiriki
vizuri katika masuala ya uzalishaji.
Ameahidi kuwa Wadau wa Maendeleo
wako tayari kusaidia jitihada hizo ili kuhakikisha kuwa Tanzania
inafikia malengo hayo kwa kuwezesha miundombinu ya ukusanyaji mapato
yake ya ndani, usimamizi na matumizi mazuri ya fedha za umma, kuiwezesha
sekta binafsi kushiriki katika miradi ya kielelezo pamoja na kusaidia
kuibua sera bora na kufadhili miradi yake ya maendeleo.
Serikali na Washirika wa Maendeleo
wamekubalina kukutana mara mbili kwa mwaka ambapo kikao kingine
kinatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2018.
No comments :
Post a Comment