Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu akizungumza na wananchi katika moja ya mikutano yake wakati wa
ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA wilayani Kahama.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu, akisisitiza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri Wilayani humo.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,
viongozi wa Halmashauri ya Ushetu pamoja na viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi baada ya kukagua kisima cha maji. (kinachoonekana nyuma yake)
Viongozi hao walimweleza umuhimu wa kisima hicho kuunganishwa na
nishati ya umeme.
Mmoja wa wananchi akieleza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza jambo katika moja ya ziara zake Wilayani Kahama
………………..
Na Asteria Muhozya, Kahama
Naibu Waziri wa Nishati Subira
Mgalu amewataka Madiwani kupitia Mabaraza yao kujadili masuala
yanayohusu Sekta ya Nishati ikiwemo kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa
Usambazaji Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Amesema endapo masuala ya Nishati
yatajadiliwa katika mabaraza hayo yatasaidia kuwepo
msukumo kwa
wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo katika maeneo yao na hivyo
kuongeza kasi ya utekelezaji wake kwa kuzingatia umuhimu wa nishati
hiyo.
Naibu Waziri Mgalu aliyasema hayo
wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA Wilayani
Kahama ambapo alitembelea Kata na vijiji mbalimbali wilayani humo.
Aidha, aliwataka Wakandarasi
wanaotekeleza miradi husika kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa za
utekelezaji wa majukumu yao katika Ofisi za Wilaya na vijiji katika
maeneo wanayotekeleza miradi hiyo.
Akifafanua zaidi kuhusu
utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Tatu alisema kuwa, Serikali
imelenga kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyosalia katika utekelezaji
wa REA awamu ya I na ya II vinafikiwa na nishati hiyo na kuongeza kuwa,
“fedha za umeme zipo lakini lazima serikali ijiridhishe kuhusu namna
mradi unavyotekelezwa”.
“Viongozi wote wakuu
wamekwishasema vijiji vyote kunakopita miundombinu ya umeme haviwezi
kukosa umeme. Kwetu sisi kuwaletea wananchi umeme ni agizo, lazima
tulitekeleze,”alisisitiza Mgalu.
Naibu Waziri aliwataka wananchi
waendelee kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika
utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya REA na kuongeza kuwa, ina
manufaa makubwa kwa taifa katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Akiwa katika Kata ya Zongomela,
Naibu Waziri alitembelea eneo kunakofanyika shughuli za uchimbaji madini
ambako aliwataka TANESCO ifikapo tarehe 2 Machi, 2018 kufanya tathmini
ya mahitaji ya umeme kwa ajili ya shughuli za uchimbaji. Awali,
wachimbao walimweleza Naibu Waziri kuwa, wanatumia majenereta kwa ajili
ya shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya wa
Kahama Fadhili Nkurlu alitoa onyo kwa wote wenye lengo la kufanya
udanganyifu wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kueleza kuwa,
watakaobainika watashughulikiwa.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi
wa REA Hussein Shemdasi aliwataka wananchi kutunza miundombinu ikiwemo
kuachana na tabia ya wizi wa mafuta ya transfoma kwa kuwa serikali
inatumia gharama kubwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Baadhi ya Kata alizotembelea wakati wa ziara hiyo ni pamoja na Kata ya Iboje, Nzogomela, Kisuke na Isaka Jana
No comments :
Post a Comment