Na Fatma Salum-MAELEZO
Serikali ya Tanzania imepokea
msaada wa Shilingi bilioni 77.3 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya
kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo (New
Bagamoyo Road) kuanzia makutano ya Morocco hadi Mwenge Jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza kwenye hafla ya
kutiliana saini makubaliano ya msaada huo iliyofanyika leo Jijini Dar es
Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James
aliishukuru
Japan kwa msaada huo ambao utawezesha upanuzi wa barabara
hiyo yenye urefu wa Kilometa 4.3 ili iweze kuwa njia nne na kuacha
nafasi kwa ajili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
“Upanuzi wa barabara hii sio tu
unapunguza foleni Jijini Dar es Salaam, bali ni kiunganishi muhimu kwa
usafirishaji wa bidhaa kati ya Bandari ya Bagamoyo na mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani na hata maeneo mengine ya nchi,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Pia Katibu Mkuu huyo alisema kuwa
Tanzania inaishukuru Japan kwa misaada mbalimbali inayotoa kwa ajili ya
kufadhili miradi mingine mingi hapa nchini ikiwemo miradi ya barabara,
umeme, kilimo na kadhalika.
Aidha aliihakikishia Serikali ya
Japan kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati yao
na kuahidi kufuatilia kwa karibu miradi yote ili kuhakikisha inajengwa
kwa ubora na kiwango kinachotakiwa.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu
kutoka Shirika la Kimataifa la misaada la Japan (JICA), Toshio Nagase
alisema kuwa shirika hilo limekuwa likifadhili miradi mbalimbali ya
usafiri Jijini Dar es Salaam ukiwemo mradi wa barabara ya juu ya TAZARA
(flyover) ambao utakamilika Oktoba mwaka huu.
No comments :
Post a Comment