Brass band ya Chipikizi
ikiongoza maandamano ya wakunga na wauguzi kupita mbele ya mgeni rasmi
Waziri Afya Mhmoud Thabit Kombo katika maadhimisho ya siku ya wakunga
Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Wasanii Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mama Mariyam Othmani Mihale
akiongoza wakunga na wauguzi katika wimbo maalum wa maadhimisho ya siku
ya wakunga Duniani katika ukumbi wa Wasanii Rahaleo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wuguzi na
Wakunga Zanzibar Amina Abdulkadir Ali akitoa maelezo juu ya siku ya
Wuguzi duniani katika maadhimisho yaliyofanyika ukumbi wa wasanii
Rahaleo.
Mwakilishi wa Shirika
linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) Zanzibar Sabina Luoga
akizungumza na washiriki wa maadhimisho hayo katika Ukumbi wa wasanii
Rahaleo Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud
Thabit Kombo akizungumza na wakunga na wauguzi walioshiriki maadhimisho
ya siku ya wakunga duniani yaliyofanyika ukumbi wa wasanii Rahaleo
Mjini Zanzibar.
Picha ya pamoja ya Mgeni rasmi
Waziri wa Afya Zanzibar na viongozi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga na
Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar katika maadhimisho ya siku ya wauguzi
duniani yaliyofanyika Rahaleo Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.
……………………
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Hospitali na Vituo vya Afya vya
Wilaya vinaweza kupunguza idadi ya akinamama kujifungulia Hospitali kuu
ya Mnazimmoja iwapo juhudi za kuandaa mazingira mazuri zitachukuliwa na
wakunga na wauguzi wa vituo hivyo.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit
Kombo ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya wakunga Duniani
yaliyofanyika Ukumbi wa Wasanii Rahaleo.
Amesema akinamama wengi
wamejenga imani ya kujifungua Hospitali kuu ya Mnazimmoja na kupelekea
upungufu wa nafasi katika Hospitali hiyo huku vituo vya Afya vijijini
vikiwa na akina mama wacheche wanaokwenda kwa huduma ya kuzaa.
Ameongeza kuwa Hospitali ya
Mnazimmoja inazalisha zaidi ya akinamama 50 kwa siku na Mwembeladu
wanawake 30 wengi wao kutoka vijijini wakati vituo vya afya vya huko
vinazallisha wanawake wawili hadi watano kwa siku.
Waziri Mahmoud amewataka wakunga
na wauguzi wa vituo vya afya vya Wilaya vinavyotoa huduma ya kuzalisha
kuandaa mazingira yatakayowavutia wanawake kujifungua katika vituo
vyao.
Amesisitiza kuwa Serikali
itaendelea na mkakati wa kuandaa mazingira mazuri na kuweka miundo mbinu
bora ikiwemo vifaa vya kisasa hivyo amewataka wafanyakazi nao
kubadilika na kuwapa faraja wagonjwa ili wajenge imani kwao.
Amesema Serikali imetoa kibali
cha kuajiri wafanyakazi wa sekta ya afya 201 kuanzia fani ya ukunga
mpaka madaktari bingwa ili kuondosha upungufu wa wafanyakazi wa kada
hizo katika Hospitali na vituo vya afya.
Amewataka wakunga na wauguzi
kujenga moyo wa upendo, huruma na kuweka mbele maadili ya kazi na
kuwahudumia wagonjwa bila ya kuwabagua kwa rangi, kabila ama nyadhifa
zao na kutumia lugha nzuri.
Aidha amewashauri kutumia fursa
walizonazo kujiendeleza kitaaluma kwa vile nafasi zipo katika vyuo vya
ndani na nje ya nchi na Wizara iko tayari kuwasaidia.
Mwenyekiti wa Baraza la Wakunga
na Wauguzi Zanzibar (ZNMC) Amina Abdulkadir Ali amesema lengo kubwa la
siku ya wauguzi Duniani ni kutoa mwamko kwa wananchi juu ya mchango wa
wakunga katika jamii na kuwa pamoja nao.
Katika risala iliyosomwa na
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wakunga Zanzibar (ZANA) Valeria Rashid Haroub
wameeleza changamoto zinazowakabili ikiwemo uhaba wa vitendea kazi
wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua na uhaba wa madaktari bingwa
katika kiliniki hizo.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo
mwaka huu ‘Wakunga, Akinama na Familia ni washirika wa kudumu’. Ukiwa na
maana ya kufanyakazi kwa karibu na familia, sio mama peke yake katika
kutunza familia pamoja na kuwalinda watoto katika afya bora na
kuwaepusha katika vitendo vya ukatili.
No comments :
Post a Comment