NA HUSNA SAIDI-
MAELEZO
CHAMA cha Kutetea
Abiria Tanzania (CHAKUA) kimeishauri Serikali kuanzisha mfumo wa kukata tiketi
kwa njia ya mtandao ili kudhibiti tiketi feki zinazotolewa na baadhi ya mabasi
yaendayo mikoani katika stendi kuu ya mabasi ya Ubungo, Jijini Dar es
Salaam.
Hayo yamesemwa na
Mwenyekiti Taifa wa CHAKUA, Hassan Mchanjama alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari kuhusu utoaji wa tiketi feki kwa mabasi yaendayo mikoani, leo Jijini Dar
es Salaam
Mchanjama alisema
kuwa, Aprili 21 mwaka huu chama hicho kiliiandikia barua Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) yenye kumbukumbu namba CHAKUA/KMN/04/2017 kuiomba
Serikali kuanzishA mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya mtandao ili kuepukana
na ubababishaji, utapeli na wizi wa kila siku unaofanywa na baadhi ya Mawakala,
Makarani na wapiga debe katika stendi zote nchini Tanzania.
“Kumekuwa na wimbi
kubwa la tiketi feki ambazo hutolewa na mawakala wa mabasi katika stendi ya
mabasi ya Ubungo na Mbeya, hiyo ni kutokana na kukamatwa kwa baadhi ya vitabu
vya tiketi ambavyo vimefojiwa TIN namba bila kibali kutoka TRA”, alisema
Mchanjama.
Aliongeza kwa kusema,
mfumo huo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya mtandao utasaidia kuokoa muda,
kuondoa kero za abiria kuibiwa, kuwabana Mawakala na Makarani ambao wamakuwa
wakitoroka na mauzo ya tiketi, wamiliki kupata pesa zao kwa uhakika, kujua
idadi kamili ya abiria waliokuwepo ndani ya basi husika, kujua idadi ya watu
waliopoteza maisha na majeruhi pindi ajali zinapotokea pamoja na kusaidia
Serikali kukusanya kodi kwa urahisi na uhakika.
Aidha, CHAKUA imefanya
utafiti kwa muda mrefu na imegundua njia pekee ya kuondoa matatizo hayo ni
kuhama katika mfumo unaotumika sasa na kuingia kwenye mfumo wa mtandao
(ki-electronic) ambao una mafanikio na ufanisi mkubwa hususani unaotumika
katika mabasi ya mwendokasi UDART (BRT).
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Katibu wa Marine, Wilson Sylvester Damo
aliwataka abiria kuwa na mazoea ya kukata tiketi kwenye sehemu husika
zinazojulikana kisheria ili kuepukana na usumbufu unaojitokeza.
Nae, Katibu Idara ya
Reli Maulid Masalu aliwataka waandishi wa habari kushirikiana kwa ukaribu na CHAKUA
kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na faida ya utumiaji wa mfumo wa kukata tiketi
kwa njia ya mtandao kwani ni salama zaidi.
No comments :
Post a Comment