Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali imejipanga kuwatoza kodi
wakazi wanaomiliki maeneo yaliyopo mijini ambayo hayana hati wala ofa
kwa viwango vile vile ambavyo wakazi wenye hati wanatozwa.
Tamko hilo limetolewa leo Jijini
Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William
Lukuvi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ulipaji wa
kodi za ardhi.
Waziri Lukuvi amesema kuwa wizara
hiyo inaendelea na ukaguzi wa ardhi ambapo mwanzoni ilianza na ukaguzi
wa mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa lakini kwa sasa imegundulika
kuwa kuna maeneo makubwa mijini yasiyokuwa na hati yanamilikiwa na
wananchi na kusababisha eneo kubwa la ardhi kutumika bila kulipiwa kodi.
“Kwa muda wote huo Serikali
imekuwa haiwatozi kodi wananchi wanaomiliki maeneo mijini bila kuwa na
hati hivyo, kuanzia sasa Serikali kupitia wizara yangu itawatoza kodi
watu wote nchini wanaomiliki maeneo ndani ya miji hata kama hawana hati
au ofa ili mradi wana karatasi za mauziano ya ardhi,”alisema Lukuvi.
Ameongeza kuwa watu wote waliopo
mjini ambao wana ardhi lakini hawana hati wala ofa wapeleke taarifa zao
za maeneo wanayoyamiliki kwa maafisa wateule wa ardhi kwenye
halmashauri zao ili yaweze kujulikana ili kuanza kulipiwa kodi.
Amefafanua kuwa kila mwananchi
lazima aende na kielelezo kinachoonyesha umiliki wake katika eneo husika
na akatamke mwenyewe ukubwa wa eneo alilonalo ili kama itatokea
amedanganya ukubwa wa eneo lake na wizara ikagundua basi eneo hilo
lililozidi litamilikiwa na Serikali bila kulipa fidia yoyote.
Aidha, Waziri Lukuvi amesema kuwa
kuanzia mwezi Julai mwaka huu wizara itaanza kuwatoza kodi wananchi
wote waliojenga mjini katika maeneo ambayo viwanja vyake havijapangwa
wala kupimwa kwani watu hao wanaishi mjini na wanatumia miundombinu ya
umma inayojengwa kwa kutumia kodi za wananchi.
“Ardhi ya Tanzania inayotumika ni
zaidi ya asilimia 70 lakini eneo linalolipiwa kodi halizidi asilimia 11
na wengi wao wanaitumia isivyo rasmi na hawalipi kodi kwa Serikali
hivyo kila mtu mwenye ardhi awe na nyaraka rasmi au isiyo rasmi wote
wanatakiwa kulipa kodi ya ardhi na baada ya miezi 6 kutoka sasa, eneo
ambalo halitakuwa limesajiliwa litachukuliwa na kumilikiwa na
Serikali,”alimalizia Lukuvi.
Ni lazima kuwatambua watu wote
wanaomiliki ardhi kisheria, kimila au kwa namna nyingine yoyote ili
kufahamu ardhi inamilikiwa na nani na inatumika kwa matumizi gani.
No comments :
Post a Comment