Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akionyesha baadhi ya nyaraka za
ardhi wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo
jijini Dar es Salaaml,kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dkt.
Angelina Mabula na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Yamungu
Kayandabila.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi imetayarisha hati 214 kwa wakazi wa Jiji la Dar es
Salaam waliosalimisha ofa zao za umiliki wa ardhi kwenye wizara hiyo ili
waweze
kumiliki ardhi hizo kihalali.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
humo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mambo mbalimbali
yanayohusu wizara hiyo.
Waziri Lukuvi amesema kuwa ni
rahisi kwa wananchi wenye umiliki wa ofa kutapeliwa kuliko wakiwa na
umiliki wenye hati ambazo ni halali hivyo ili kuondoa changamoto hiyo
wizara ilitoa muda kwa wananchi kupeleka ofa hizo ili watayarishiwe hati
halali.
“Kuwa na umiliki halali wa ardhi
ni jambo kubwa kwa usalama wa wananchi wenyewe, nataka ifike siku
Tanzania iwe haina mtu anayemiliki ardhi kwa kutumia ofa kwa sababu sasa
hivi wizara haitoi ofa, ofa hizo zilishakoma siku nyingi,”alisema
Lukuvi.
Ameongeza kuwa ingawa muda wa
kusalimisha ofa hizo za umiliki umekwisha lakini wizara hiyo inatoa muda
zaidi kwa watu ambao bado hawajapeleka ofa zao katika Halmashauri zao
za wilaya kupeleka ofa hizo ili waweze kumiliki ardhi hizo kwa hati.
Aidha, akiongelea kuhusu
utayarishaji wa teknolojia itakayohusika na masuala yote ya ardhi
inayojulikana kama ‘Mfumo Unganishi wa Ardhi’, Waziri Lukuvi amesema
kuwa tayari Kampuni ya Kifaransa iliyoshinda tenda inaendelea na kazi na
mnamo Julai mosi mwaka huu hati ya kwanza ya kielektroniki ya mfano
itatolewa.
Tayari jengo litakalotumika kwa
ajili ya shughuli hizo limeshakamilika na mfumo huo bado unaendelea
kutengenezwa ili kuwezesha wananchi wote wanaomiliki ardhi Tanzania
wanamilikishwa hati za kielektroniki.
No comments :
Post a Comment