NA Beatrice Lyimo-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
TANZANIA Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Mahakama kukusanya
Shilingi Trillioni 7.3 ambazo ni matokeo ya serikali kushinda kesi
mbalimbali za ukwepaji kodi.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo
jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Sheria na Mwaka
mpya wa Mahakama iliyobeba kauli Mbiu isemayo Utoaji haki kwa wakati
kuwezesha ukuaji wa uchumi.
Alisema kuwa Takwimu zinaonesha
kuwa kumekuwa na baadhi ya kesi za pingamizi za kodi ambapo Serikali
imeshinda kesi hizo japo fedha hizo hazijakusanywa mpaka sasa.
“Kukwepa au kutolipa kodi ni kosa
kubwa sana, kila mtu anawajibu wa kulipa kodi nchini kwa maendeleo ya
nchi” nalifafanua Dkt Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa
katika kuelekea ukuaji wa uchumi, Mahakama iwe sehemu ya chanzo cha pato
la taifa kwa kwa kuhakikisha wale wanaotakiwa kulipa fidia baada ya
kushindwa kesi wanafanya hivyo pamoja na kuwabana wakwepa kodi kwani
kutimiza hilo kutaleta mabadiliko katika uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine Rais
Magufuli alisema kuwa Maendeleo ya nchi hayaangalii chama chochote,
hivyo amevitaka vyombo vya utoaji haki kutoa haki kwa usawa.
Kwa upande wake Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania Profesa Ibrahim Juma alisema kuwa Mahakama imeandaa Mpango
mkakati uliolenga kufanya maboresho ndani ya Mahakama.
Alisema kuwa mpango mkakati huo
umelenga masuala makuu matatu ikiwemo Utawala bora, uwajibikaji na
usimamizi wa rasilimali, upatikanaji wa haki na kwa wakati, uimarishaji
wa amani kwa wananchi na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za
mahakama.
Aidha Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakama imefanikiwa kusikiliza mashauri ya kesi za uchaguzi kwa asilimia 100.
“kati ya mashauri ya kesi 249
ikiwemo 53 za ubunge na 196 za madiwani ya waliopinga uchaguzi kati ya
kesi hizo, kesi 52 za ubunge zilikamilishwa na kesi zote za madiwani
zilikamilishwa” alifafanua Kaimu Jaji Mkuu.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali
George Masaju amesema kuwa Katiba imeanisha bayana Kanuni ambazo
zinapaswa kuzingatiwa na Mahakama wakati ikitekeleza mamlaka yake ya
utoaji haki.
“utoaji haki mapema ipasavyo ni
moja ya Kanuni ambazo Mahakama inapaswa kuzingatia katika utekelezaji wa
majukumu yake kama inavyoelekezwa katika Katiba” alifafanua Mwanasheria
Mkuu.
Alisema kuwa Serikali imeendelea
kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara katika nchi ya
Tanzania hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Siku ya Sheria nchini ilioanzishwa mwaka 1996 ikiwa ni siku muhimu ya kuombea Majaji na Mahakimu ili kuweza kusikiliza kesi.
No comments :
Post a Comment