Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo
Mifugo na Uvuvi Mhandisi Mathew John Mtigumwe akisisitiza jambo wakati
wa kikao cha pamoja na wafanyakazi wa wizara hiyo
Watumishi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza kwa makini Katibu mkuu wa wizara hiyo Mhe Mhandisi Methew Mtigumwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo
Mifugo na Uvuvi Mhandisi Mathew John Mtigumwe hii leo amewaondoa hofu
watumishi wa wizara yake kuhusu zoezi la serikali kuhamia Dodoma kuwa
litafuata misingi na stahili za watumishi kwa mujibu wa kanuni za
utumishi wa Umma.
Mhandisi Mtigumwe ametoa kauli
hiyo wakati wa kikao maalumu cha kuhusiana na uamuzi wa serikali kuhamia
Makao Makuu ya Nchi mkoani Dodoma kilichokuwa na lengo la kujadili kwa
pamoja namna ya utendaji kazi katika wizara hiyo sambamba na kutoa
utaratibu utakavyokuwa kuelekea mjini Dodoma.
Mtigumwe amebainisha kuwa Awamu ya Kwanza ya uhamisho
utawahusisha watumishi 88 kutoka Idara Kuu ya Mazao, ambapo katika
mchakato huo watumishi 41 watahamia Dodoma kuanzia tarehe 14 – 15/2/2017
na wengine 47 waliobaki watahamia muda wowote katika kipindi cha
kuanzia mwezi Februari hadi kufikia mwezi Juni.
Mtigumwe amewaeleza watumishi hao kuwa maandalizi ya ofisi za
Wizara ya kilimo zilizopo mjini Dodoma zinaendelea vizuri na tayari
baadhi ya maeneo yamekamilika huku mengine yakiendelea kukamilishwa ili
kukidhi matakwa kwa ajili ya watumishi wote watakapohamia mjini Dodoma.
Uamuzi wa Watumishi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuhamia
mjini Dodoma ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuitaka Serikali yote kuhamia
Dodoma ili kutekeleza uamuzi uliofikiwa tangia miaka ya 70 na Serikali
ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere kutambua na kutangaza kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.
Mhandisi Mtigumwe amebainisha hayo hii leo katika kikao cha
pamoja na watumishi wa wizara ya kilimo katika Mkutano huo ulifanyika
Makao Makuu ya Wizara hiyo Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
No comments :
Post a Comment