Thursday, January 5, 2017

MAHOJIANO YA MHESHIMIWA HAMAD RASHID MOHAMMED KUHUSU MIAKA 53 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR


hamada
Na  Habari MAELEZO
Katika kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Idara ya Habari – MAELEZO ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mwenye dhamana ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Hamad Rashid Mohammed, kuhusiana na maadhimisho hayo. Yafuatayo ni maswali na majibu katika mahojiano hayo:
SWALI: Zanzibar imetimiza miaka 53 ya Mapinduzi una lipi la kuwaeleza Wazanzibar?
JIBU:

Unapoongelea Mapinduzi ya Zanzibar, wote tukumbuke ndio chanzo cha Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, bila Mapinduzi Muungano usingekuwepo, haya yote ni katika kuzingatia umoja. Umoja ni jambo la msingi sana kwa Wanzanzibar kwa kuwa Serkali ya Kikoloni ilitubagua na kupanda mbegu ya kubaguana hata kwa sisi Wafrika wenyewe.
Ni vema kuyaenzi Mapinduzi haya kwa kuwa ndio chanzo cha Muungano wetu, Amani yetu, Umoja wetu, Utulivu wetu na Mshikamano wetu. Hivyo tunakila sababu ya kushukuru uwepo wa Mapinduzi ya mwaka 1964 yameweza kutuunganisha tukawa na Umoja.
Awamu ya kwanza ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Marehemu Shekhe  Abeid Amani Karume alifanya mambo mengi makubwa mfano ujenzi wa nyumba bora za makazi za wananchi,  kutoa elimu bure, huduma za afya, maji  na kufuta kabisa ubaguzi wa kila aina ambao ulikuwa umeota mizizi hapa Zanzibar kabla ya Mapinduzi.
Aidha, Awamu ya pili Serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Marehemu Abood Jumbe, iliandika Katiba ya Zanzibar, kuundwa kwa Baraza la Wawakilishi, kutengeneza muundo wa Baraza la Wawakilishi na kuanza kazi kwa kuwa na wakikilishi Zanzibar na Katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu ya tatu mpaka ya Saba ni muendelezo wa:
Tatu, Uchumi wa Zanzibar umekua, kama kuzalisha mazao zaidi hapa visiwani, mfano asilimia 80 ya matunda yalikuwa yanatoka Tanzania Bara lakini sasa katika Awamu ya saba ya Mheshimiwa Dkt Ali Mohammed Shein, uzalishaji wa matunda umeongezeka asilimia 80 inatoka Zanzibar na 20 tu ndio yanatoka Tanzania Bara.
Ujenzi wa barabara kila mkoa, miundombinu mbalimbali imeongezeka kama hospitali, bandari imeimarishwa ambapo kwa sasa kuna meli nyingi zaidi za mizigo na Uvuvi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Nne, suala la kubadilishana uongozi kutoka awamu ya kwanza mpaka ya saba, tofauti na uongozi wa kisultani ambao ulikuwa ni wakurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine katika familia moja tu.
SWALI: Mheshimiwa Hamad Rashid wewe ni kati ya watu wachache waliobobea katika siasa na umeitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na Bunge la  Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Unadhani muelekeo uliopo mpaka sasa unaleta hali halisi ya matarajio ya Mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1964?
JIBU:
Muelekeo upo na madhumuni makubwa ya mapinduzi ni kutaka kujitawala wenyewe, unapojitawala utaepuka kudharauliwa, kunyanyaswa na kuondoa ubaguzi uliokuwa umekidhiri katika utawala wa Wakoloni enzi hizo.
Pili makazi na maisha ya Wanzanzibar waliowenngi yalikuwa duni na umaskini ulikuwepo wa hali ya juu kwa jamii za kiafrika na; Tatu Uchumi wa Zanzibar ulikuwa mikononi mwa wakoloni hakuna Mzanzibar aliyeruhusiwa kumiliki sehemu ya uchumi wa nchi. Kutokana na kadhia hiyo utamaduni wetu ulidharauliwa utu wetu ulipuuzwa na ushiriki wetu wa uchumi ulikuwa haupo.
 Hivyo madhumuni makubwa ya mapinduzi ni kuleta umoja, usawa, utulivu na mshikamano miongioni mwa wanzanzibar hilo limefanikiwa kwa asilimia kubwa ukilinganisha na hali ya mwaka 1964.
SWALI: NIni maoni yako kuhusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanznibar kuelekea kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa?
JIBU:
Tukubali kuwa uchumi ndio msingi wa maendeleo wa Taifa lolote. Sera zinazoandaliwa ni lazima zilenge katika kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi. Rais anaposema anataka Taifa liondokane na umasikinini ni kweli tutaondokana nao, kama tutakuwa na viwanda vichache vyenye manufaa kwa nchi kwa kuwa eneo la kisiwa ni dogo. Hivyo, tutaongeza ajira Wakulima watapata soko la uhakika la mazao yao na bidhaa zitakazozalishwa zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa kuwa zimeongezewa dhamani.
Ni vema Wazanzibar tukadhamini vitu vinavyozalishwa nchini mwetu na kupenda kushiriki katika kufanya kazi.
SWALI: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalipi la kujivunia katika miaka 53 ya Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar?
JIBU:
Yapo mengi ya kujivunia, leo hii hakuna wakutupuuza, kutudharau na kutunyanyasa, tunatembea kifua mbele kwa marefu na mapana katika kila jambo liwe lakijamii, kiuchumi, elimu, miundombinu, afya, michezo au utamaduni kila Mzanzibar ana haki ya kushiriki katika maendleo ya Zanzibar. Hapa la msingi kila Mzanzibar ajiulize atafanya lipi kwa Zanzibar ili kuleta maendeleo, kila raia anatambua maendeleo yetu yataletwa na sisi wenyewe. Maana ukitaka au kudai haki lazima ujue wajibu wako kwa nchi katika kuleta maendeleo.
Mambo ya msingi ya kujivunia yanabaki kuwa ni Umoja wetu, Mshikamano wetu Amani yetu, Utulivu wetu  na hali ya kuvumiliana katika siasa hasa uvumilivu wa kufanya siasa za vyana vingi.
SWALI: Suala la Nidhamu kwa Watumishi wa Umma, Taasisi, Mashirika na Idara za Serikali linatiliwa mkazo sana na Rais wa Zazibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein hili unalizungumziaje?
JIBU:
Ni kweli Mheshimiwa Rais Dkt. Ali Mohammed Shein, anasisistiza nidhamu na kufanya kazi kwa bidii na kujituma. Amesema kabisa hataki tufanye kazi kwa mazoea, anasisistiza kabisa kwenda kwa wananchi na kufanya kazi nao ili kujua wanachofanya, changamoto zao ili viongozi waweze kuzitatua pamoja na wananchi. Anatuhimiza tutoke tuende kwa wananchi na kuona ni jinsi gani tunaweza kufanya nao kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo bila kubagua rangi, kabila, dini, Jinsia na uwezo.
ADC tunasema asilimia 70 kazi na asilimia 30 tutakaa maofisini. Kwa sasa watumishi wote waone umuhimu wa kufanya kazi badala ya kupiga maneno maneno tu, tabia hii haitatusaidia Wazanzibar.
SWALI: Nini nafasi ya Vyama vya Upinzani katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar?
JIBU:
Vyama vya Upinzabni vina nafasi kubwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na nje ya serikali katika masuala muhimi kwa wananchi ya kuleta maendeleo. Nitakupa mfano binafsi na chama chetu cha “Alliance for Democratic Change” – ADC tulishirikiana na wananchi kutafuta wafadhili kama chama cha siasa na kujenga uwanja wa mpira Pemba sikuwa Waziri wala Diwani.
Pia ni fadhaa kumsingizia Mheshimiwa Rais eti hatoi nafasi kwa vyama vingine vya siasa. Mimi mwenyewe nipo ndani ya serikali tunakaa kwenye vikao mpaka saa 6 usiku kila mhusika natoa mawazo yake katika kuwaletea maendeleo Wazanzibar. Kama hoja unayotoa ni ya msingi lazima itakubalika, inapofikia suala la maendeleo Mheshimiwa Rais Shein haangalii chama anaangalia masilahi ya Zanzibar kwanza.  
Kila Mzanzibar ana wajibu wa kujiuliza ameifanyia nini Zanzibar ili kuleta maendeleo na sio kusifiwa kwa malumbano ambayo hayana masilahi kwa maendeleo.
SWALI: Ni kweli Serikali ya SMZ Ikiongozwa na Chama cha Mapinduzi – CCM inakandamiza demokrasia na kubagua Vyama Vingine vya siasa?
SWALI: Ni kweli Serikali ya SMZ Ikiongozwa na Chama Tawala cha CCM inakandamiza demokrasia na kubagua Vyama Vingine?
JIBU:
Hili la kubaguliwa na kukandamizwa demokrasia halina ukweli hata kidogo, Katika Awamu ya kwanza ya uongozi niliwahi kupendekeza jambo ambalo idadi kuwa ya washiriki walilikataa, lakini kutokana na uzito wa hoja, Serikali ililipima na kulichukua hii ndio demokrasia, kama suala lina masilahi kwa nchi ni vema likafanyika kwa masilahi ya nchi.
Mimi ni mwanachama wa “Alliance for Democratic Change” katika utendaji wa kazi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Shein sijawahi kubaguliwa au kutengwa kwa sababu natoka chama kingine cha sIasa.
Mhe. Rais anatushirikisha katika kila jambo na katika vikao tunaongea na kutoa mawazo na mapendekezo yetu ambayo yanachukuliwa na kufanyiwa kazi kama ambavyo yangeweza kutolewa na muwakilishi wa chama chake cha CCM.
SWALI: Una wito gani kwa wanzanzibar na Watanzania kwa ujumla?
JIBU:
Mosi, Umoja wetu, Usawa kwa kila Raia na Mshikamano wetu ni masuala ya msingi sana katika nchi yetu.
Pili, tunataka nchi hii ibaki salama, mnapokuwa na amani katika nchi yenye rasilimali za kutosha mtaweza kujipanga vema na kuzitumia rasilimali hizo kwa faida ya wote, hivyo  ni lazima tuhakikishe kuna Amani na pale wachache wanapohatarisha amani hiyo kwa pamoja tushirikiane kusuluhisha ili kurejesha hali ya utulivu na amani.
Serikali ipo imara katika kuleta Maendeleo lakini wewe Mzanzibar ni lazima utimize wajibu wako. Mfanya biashara alipe kodi na afanye biashara ya halali. Mkulima afanye kazi kwa bidii na Serikali ihakikishe inampatia pembejeo kwa wakati na zenye ubora.
Tatu, sisi wanasiasa njia za kurekebisha makosa zipo tukubali kukaa chini na kuzungumza, lawama hazina nafasi, Chama cha siasa ni lazima kuwa na mipango ya maendeleo na mipango hiyo ifanyike hata kama hauko katika uongozi.
Nne, tunao viongozi wetu wa dini kama Mashekhe, Mapadri Wachungaji tuwe karibu nao tuongee nao waweze kutuelekeza pale tunapokosea na kwenda katika mwenendo sahihi. Mwisho nawapongeza kwa dhati kabisa Wazanzibar kutimiza miaka 53 ya Mapinduzi.

No comments :

Post a Comment