WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema atamuita Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Bw. Hassan Jarufo ili
aje amueleze ni kwa nini wakulima wa zao hilo wanacheleweshewa malipo
yao kinyume na maagizo ya Serikali.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada
ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea.
Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa
kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Niliagiza wanunuzi waje na
bond (dhamana ya mauzo), waziweke benki ndipo waingizwe kwenye mnada.
Kwa maana hiyo mnada ukimalizika, benki inakata fedha husika na kuingiza
kwenye chama cha wakulima.”
“Hapa tatizo ni kwamba
hatukusimamia vizuri zuala hili. Tulipaswa tujiridhishishe kwanza kama
mnunuzi amelipa fedha benki. Tatizo la biashara hii watu wengi ni
madalali, wanaangalia hali ikoje na wakibaini kuna cha juu, ndiyo
anaagiza na kuamua kuja kulipa. Kama angekuwa amelipa benki, ile hela ya
awali ingekatwa katika fedha ya dhamana aliyokwishaitoa,” amesisitiza.
Oktoba 16, 2016 wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja
cha Sokoine wilayani Nachingwea, mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema
alishatoa maelekezo tangu Aprili, mwaka huu kwamba wanunuzi wa korosho
ni lazima watoe asilimia 25 ya malipo wanayotaka ili kuepuka tatizo la
madalali kuingilia kati biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi na Wakuu wote wa
wilaya za mkoa huo wawahimize wakulima wapande miche mipya ya korosho
kwa sababu mikorosho iliyopo imezeeka na haitoi mazao ya kutosha.
“Mnatakiwa muwahimize wananchi
wapande miche mipya mara tu mvua zitakapoanza ili ianze kukua wakati
wakusubiria kung’oa ile ya zamani. Nimeambiwa korosho bora hazipaswi
kuzidi punje 190 ili zijae kwenye kilo moja. Ubora wa miti ya korosho
ukishuka na idadi ya punje pia inapungua,” amesema.
Amesema kigezo kikuu cha
ununuzi wa korosho hivi sasa ni idadi ya punje na kwa Ruangwa na
Nachingwea, idadi inakuwa kubwa kwa sababu punje zake ni ndogo. “Wenzetu
wa Tandahimba walipanda miche mipya tangu miaka minne iliyopita kwa
hiyo sasa hivi wanavuna korosho zenye ubora,” ameongeza.
Amempongeza Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba kwa uamuzi wake wa kuvunja mfuko wa
wakfu wa korosho (CIDTF) na akamtaka afute mifuko kama hiyo kwenye mazao
mengine kama katani, chai na kahawa kwani inafanya kazi ambazo zinaweza
kufanywa na bodi za mazao hayo.
“Waziri Tizeba alishaanza na
zao la pamba, sasa aende kwenye mazao mengine ili fedha ambazo watu wa
mfuko huu walikuwa wakizitumia kulipana posho tu, sasa ziende kwenye
bodi kuhamasisha wakulima walime zaidi na ikibidi wapewe hata mashine za
kupulizia dawa,” ameongeza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, DESEMBA 27, 2016
No comments :
Post a Comment