Wednesday, November 2, 2016

Hifadhi ya jamii kuifanya Tanzania nchi ya viwanda

  Christian Gaya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Meneja Mkuu wa Malipo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Francis Mcharage cheti cha kuthamini michango   ya wafanyakazi wa shirika hilo kwa NSSF kila mwenzi  wakati alipofungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha  (AICC) Oktoba 20, 2016.  Watatu kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na wapili kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe.
 
 
Hifadhi ya jamii ni chombo muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi na hivyo basi kusaidia kupunguza umaskini nchini kwa kutumia michango inayokusanywa na kuwekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo na hivyo kuongeza ajira na kuchochea kukua kwa uchumi wa nchi.

Maneno haya yalitamkwa na mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa sita (6) wa wadau wa NSSF, kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha, Oktoba 20, 2016. 

Kauli Kuu ya mkutano huu wa mwaka ya wananachama na wadau wa NSSF ilikuwa ni  “Hifadhi ya Jamii na Maendeleo ya Viwanda; Mweleko katika Kukuza Uchumi na Ajira Tanzania” 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa alisema amefurahishwa sana na kauli mbiu hii kwani inaendana na matarajio na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kujenga Tanzania mpya yenye uchumi wa viwanda.

“Nyote  mnamfahamu kuwa wakati wa kampeni za uchanguzi mkuu mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwaahidi watanzania kuwa serikali yake itahakikisha inajenga taifa lenye uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda na sasa utekelezaji wa ahadi hiyo umeanza kwa kasi kubwa” Waziri Mkuu alisema

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuona nchi yetu inapata maendeleo ya haraka kwa manufaa ya Watanzania wote. Aidha, katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2015 pamoja na Ilani ya Uchaguzi wa Chama Tawala Serikali imelenga kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati wenye kujengwa na viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu na kupunguza umasikini.

“Nimefarijika sana kuona kwamba NSSF imedhamiria kwenda na mweleko huo kwa kupanua wigo wa uwekezaji wake na kuelekea katika viwanda jambo ambalo litaongeza, ajira, uzalishaji na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. Maamuzi haya yataiwezesha NSSF na mifuko mingine kupata wanachama wapya na kukusanya michango zaidi na kuiwekeza ili kuweza kutimiza lengo lake la msingi la hifadhi ya jamii. 

Mtakumbuka kuwa mheshimiwa Rais Magufuli aliwahi kutoa maelekezo hayo mwezi Mei, 2016 alipokuwa akifungua majengo ya vitega uchumi vya Mfuko wa Pensheni wa (PPF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) yaliyopo hapa jijini Arusha. Mheshimiwa Rais aliagiza mifuko yote ya hifadhi ya jamii kuwekeza katika miradi inayozalisha ajira nyingi, faida ya haraka na kuchangia kiasi kikubwa katika pato la taifa hususani viwanda”  Waziri Mkuu alikumbusha. 

Alisema mkurugenzi mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara amekumbusha ya kuwa nchi yetu katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru mwaka 1961 ilikuwa na uchumi wa viwanda na kwamba mpaka hadi kufikia miaka ya 70 nchi yetu ilijitosheleza kwa kila kitu kuanzia vifaa vya shule kama madaftari, kalamu, karatasi, na vifaa vya ujenzi na tumekumbushana baadhi ya viwanda vilivyokuwepo kama vile urafiki, Sungura, Kiltex, Ubungo Spinning, Mutex, VOIL, Tabora Textile, Southern Paper Mills (Mgololo) na vingine vingi vilivyokuwa vinaendeshwa na watanzania na kuwapa watanzania ajira. Kwa sababu mbalimbali ikiwemo uwajibikaji mbovu na ubadhirifu, viwanda hivi havipo tena. 

“Jambo hili la kuwa na viwanda halafu baadaye vifungwe kwa sababu rahisi tu halitakuwa na nafasi tena kwa Serikali ya Awamu hii ya Tano na natumaini hata awamu zijazo. Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watendaji wabadhirifu na wasio kuwa na uchungu na nchi yao. Utaratibu huu ni endelevu kwa kila sekta bila kujali wadhifa wa mtu kwani wadhifa huo ulitolewa kwa lengo la kuwahudumia watanzania hivyo mtu akishindwa kutekeleza wajibu huo ni vema atupishe” Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa alisisitiza.

“Nawapongeza NSSF sana kwa juhudi zenu ambazo zinaunga mkono dhamira ya serikali ya kujenga uchumi imara kupitia uwekezaji katika viwanda. Jambo muhimu kwenu ni kusimamia kikamilifu dhamira hii” Waziri Mkuu aliwapongeza kwa dhati.

Alisema kazi ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kufanywa kwa namna mbili, kwanza ni kwa kuvifufua vilivyokuwepo na pili ni kwa kuvianzisha viwanda vipya. 

“Wenzetu wa NSSF wameanza kutekeleza yote mawili. Hilo la sukari ambalo linafanywa kwa ushirika wa PPF lakini pia NSSF wameanza kazi ya uwezeshaji kwa kutoa mikopo kwa viwanda nchini kwa dhamira hiyo hiyo ya kuijenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda. Tumeambiwa hapa ya kuwa shirika limetoa mkopo wa shilingi bilioni 3.1kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa viwatilifu yaani biolovecides katika kiwanda kilichopo Kibaha kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa biashara ya nafaka mchanganyiko kupia bodi yake (CPB)” Waziri Mkuu alisema.  

Juu ya mwelekeo huu wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kujenga Tanzania mpya yenye uchumi wa viwanda Waziri Mkuu alimalizia kwa kutamka kama yafuatayo

“Natoa Rai kwa Taasisi ambazo zimenufaika au zitanufaika na mikopo hii, kutumia kwa malengo yaliyokusudiwa na pia kurejesha kwa wakati kwa mujibu wa mikataba ili wengine nao wanufaike. Aidha, natoa wito kwa Taasisi na Makampuni mbalimbali kuiga mfano wa NSSF na PPF kuunganisha nguvu zao katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais la kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda”.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment