Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akitaza mashine ya CT Scanner wakati
alipotembelea na kukagua ujenzi wa Kampasi Mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) eneo la Mloganzila jijini Dar es salaam
Septemba 2, 2016. (PICHA
NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iweke mpango maalumu wa
kuongeza wataalamu zaidi katika sekta ya afya ndani ya nchi ili kuipunguzia
Serikali gharama za kusomesha wataalam hao nje ya nchi.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa,
Septemba 2, 2016) wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya
Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ujenzi wa Kituo cha Tiba cha Kimataifa cha
Muhimbili katika eneo la Mloganzila.
Amesema Serikali zilizotangulia zimefanya kazi kubwa na nchi
imefikia hatua nzuri ya kuongeza wataalam ndani ya nchi ambao watakwenda
kutatua changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa kwenye hospitali za mikoa na
wilaya.
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha tiba cha kimataifa
pia utawapunguzia wananchi adha ya kutafuta fedha za kwenda kupata matibabu nje
ya nchi. Tayari upasuaji mkubwa wa magonjwa ya moyo umeanza kufanyika nchini.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,
Bw. Humphrey Polepole awasake watu wote waliohusika na wizi wa lita
1,000 za mafuta ya kuendeshea mitambo katika karakana ya mkandarasi anayejenga
Kampasi hiyo.
“Wafanyakazi waache wizi. Lita 1,000 zinaondokaje katika karakana
ya mkandarasi? Hii kampuni inayolinda kama imeshindwa kazi iondolewe na Mkuu wa
wilaya usimhurumie mwizi,” amesisitiza.
Kwa
upande wake Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kukamilika kwa kampasi ya
Mloganzila kutasaidia upatikanaji wa madaktari bingwa wengi nchini ambao
watapunguza gharama za kupeleka wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Awali,
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Ephata Kaaya alisema kukamilika kwa hospitali pamoja na
kampasi yote ya chuo kutawezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa wataalamu
wa afya nchini.
Amesema hospitali hiyo itatumika kutoa huduma za afya za kitaalam
zaidi kwa magonjwa mbalimbali, hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa
nje ya nchi kwa matibabu. Pia itapunguza msongamano wa wagonjwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ujenzi wa mradi huo umegharimu Dola za Kimarekani milioni 61,
ambapo Serikali imetoa Dola milioni 18 na Serikali ya Korea imetoa mkopo wa
Dola milioni 43. Kukamilika kwa ujenzi wa kampasi hiyo ya Mloganzila
kutawezesha chuo kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa fani ya
afya kutoka 4,010 hadi 15,000.
Prof. Kaaya amesema mkataba wa awamu ya kwanza ya
ujenzi wa mradi huo ulisainiwa tarehe 12, Desemba, 2014 na ujenzi ulianza mwezi
Julai, 2015 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza taarifa kuhusu ujenzi wa
Kampasi Mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya wakati
alipokagua ujenzi huo eneo la Mloganzila jijini Dar es salaam
Septemba 2, 2016. Kulia kwake ni Waziri wa Elimu, Sayansi,
Tekinolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ufungaji vifaa vya tiba wakati
alipotembelea na kukagua ujenzi wa Chuo wa Kampasi Mpya ya Chuo Kikuu cha
Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) eneo la Mloganzila jijini Dar es
salaam Septemba 2, 2016. Kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo
hicho, Profesa, Ephata Kaaya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiondoka baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Kampasi Mpya ya Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) eneo la Mloganzila
jijini Dar es salaam Septemba 2, 2016. Kulia kwake ni Waziri
wa Elimu, Sayansi, Tekinolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na kushoto
kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Humphrey Polepole
No comments :
Post a Comment