Thursday, October 8, 2015

Changamoto za mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii







Siku ya mahafali. Mfumo wa hifadhi ya jamii unaonufaisha wigo mdogo wa nguvukazi kwa sehemu kubwa ya gharama ya sekta isiyokuwa rasmi na ambao hawana kazi ambapo idadi kubwa wakiwa vijana waliaomaliza elimu ya shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu nchini

Wiki iliyopita tuligusia baadhi ya mambo yanayosababisha kuwagusa sana wachangiaji wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii hasa pale wanapokuwa wanapoteza uanachama na kinga yao ya hifadhi ya jamii pale wanaondoka au kuhamia mfuko mwingine wa pensheni ya hifadhi ya jamii wakiwa ndani ya nchi na akivuka mpaka na kwenda nchi nyingine.
 
Lakini kuna mifano kutoka katika nchi fulani za kiafrika ambazo zimefanikiwa kutekelezwa katika bara hili la Afrika kwa kutumia kanuni zinazokubalika hapa ulimwenguni, mfano mzuri ni pale kama nchi jirani zetu za Zimbabwe na Malawi jambo kama hili la kuhamisha kinga ya hifadhi ya jamii mtu akivuka mpaka na kwenda nchi nyingine pale wanapoondoka au kuhamia mfuko mwingine wa hifadhi ya jamii hufanyika bila usumbufu na hivyo bila kupoteza uanachama na kinga yake ya hifadhi ya jamii.

Jambo la tatu ni kwamba, mfumo wa pensheni wa hifadhi ya jamii umekuwa ni eneo ambalo imekuwa na ufahamu mdogo wa kujaribu kuelezea mfumo kamili juu ya sera za jamii ambazo zinaweza kuungana na kuhusiana na sera za kiuchumi za nchi husika. Kwa mantiki hii hivyo kuna haja kubwa ya kuweka msukumo mkubwa kati ya sera za kijamii na sera za kiuchumi ili kufanya kazi kwa pamoja lengo likiwa ni kuleta mabadiliko ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Lengo la sera za kijamii na hata kwenye malengo ya milenia kwa nchi ya Tanzania hasa katika eneo la mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii iwe ni kupunguza na kuondoa umasikini na ubaguzi, na kusaidia lengo la kukuza uchumi wa nchi  na kuwa na msingi mkubwa wa kodi kwa ajili ya mapato ya serikali.

Hata hivyo bado mfumo huu unachangia sana kuleta tofauti kubwa za kijamii, na hata kati ya wanachama wenyewe kwa wenyewe. Kwa sababu mafao yanayotolewa na jinsi ya kukokotoa pensheni unafuata wastani wa mishahara mizuri mitatu ya mwisho ya mfanyakazi ya mwezi, na idadi kubwa ya wafanyakazi ni wa kima cha chini na anapofikia kustaafu hupata pensheni ya chini zaidi na zaidi ukilinganisha na mfanyakazi aliyekuwa akipata mshahara wa kima juu zaidi yake kwa mwezi. Na hii inaonesha au kudhihirisha wazi ya kuwa michango ya wafanyakazi wa kima cha chini ambao ndio wengi zaidi inasaidia kuwalipia pensheni kubwa wafanyakazi wa kima cha juu zaidi.

Lakini pamoja na hayo, picha inaonekana wazi ya kuwa kuna ongezeko kubwa la sekta isiyokuwa rasmi na mfumo wa watu wengi kutokuwa na kazi, wakati huo huo sekta iliyo rasmi ikiwa kwa ujumla inadidimia kila siku kukicha, na hata ushahidi unaonesha ya kuwa karibu idadi kubwa ya wafanyakazi ambao ni wanachama wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii wanazidi kuondoa michango yao na kukimbilia kujiunga na sekta isiyo rasmi.

Kushikiria kwa makini kwa ajili ya kuboresha mabadiliko ya manufaa ya mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya mfumo unaonufaisha wigo mdogo wa nguvukazi kwa sehemu kubwa ya gharama ya sekta isiyokuwa rasmi na ambao hawana kazi ambapo idadi kubwa wakiwa vijana waliaomaliza elimu ya shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu nchini kwa kweli hili ni jambo lisilokuwa la usawa na kutovumilika ambapo moja kwa moja linaonesha kumwelekeza na kuisukuma serikali kuwa angalifu pamoja na wadau wengine wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini juu ya idadi kubwa ya watu kuwa na kinga ndogo ya hifadhi ya jamii. Hivi karibuni, ingawa ni Afrika na sehemu zingine katika ulimwengu unaoendelea, ubunifu na njia za kusadiana pamoja zimekuwa zikichukuliwa na kufanyiwa kazi kwa ajili ya kupanua kinga ya hifadhi ya jamii kwenye sekta isiyo rasmi.

Mwisho, sababu kwa nini mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii hapa nchini mara kwa mara imekosa uaminifu na shukrani kutoka kwa wanachama na wadau wengine, hii inaonesha wazi ya kuwa kumekosekana na viwango vinavyotakiwa taasisi hii ya sekta ya hifadhi ya jamii na serikali kuvitumia katika uendeshaji na utendaji wa kila siku kama vile viwango vya huduma bora kwa wateja

Inapendekezwa ya kuwa, kwa ajili ya kushawishi kuleta maendeleo nchini kuna haja kubwa kupanga viwango vinavyotakiwa katika ngazi ya nchi na hata katika ngazi ya Afrika Mashariki kwa kutumia mfumo wa haki za binadamu, kwa kutumia mwongozo wa viwango vya jumuiya ya Afrika Mashariki na kutumia viwango vya Kimataifa huenda vikasaidia sana kukubalika kwa mfumo wa pensheni wa hifadhi ya jamii katika nchi zetu za Afrika Mashariki

Christian Gaya ni mwanzilishi wa kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa barua pepe: gayagmc@yahoo.com na kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni  simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment