Wednesday, December 26, 2012

Mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii na baadhi ya changamoto zake


Majira Jumanne Desemba 25,2012



Hifadhi ya jamii ni chombo cha usimamizi na udhibiti wa kuwakinga raia dhidi ya majanga ya kijamii. Huu mfumo umekuwepo hapa nchini Tanzania umedumu hata kabla ya ukoloni Ambapo maelezo mengi ya sera za hifadhi ya jamii zilikuwa zikiundwa na sheria mbalimbali zilipitishwa juu ya hifadhi za jamii kwa ajili ya kuwakinga jamii dhidi ya majanga mbalimbali kama vile kuumia ukiwa kazini, uzee na kupoteza kazi iliyokuwa inakupa mapato ya kukuwezesha kuishi. 


Baada ya uhuru sheria nyingi ziliundwa na zingine zilirekebishwa upwa. Hizi zikiwa pamoja na sheria namba 57 ya 1962 ya severance allowance; Mfuko wa taifa wa akiba ya wafanyakazi yaani National Provident Fund NPF) sheria namba 36 ya mwaka 1964  iliyorekebishwa chini ya sheria Namba 2 ya mwaka 1975 ya kuwa shirika la umma ambayo baadaye ilibadilishwa kuwa mfuko kamili wa hifadhi ya jamii yaani National Social Security Fund (NSSF) sheria namba 28 ya mwaka 1997 unaoendeshwa kwa utaratibu wa sheria za pensheni za bima; Pensheni za mashirika ya umma Parastatal Pensions Fund (PPF) ya kifungu cha sheria namba 14 cha mwaka 1978;

 Hizi zikiwa kama vile Master and Native Ordinance Cap 78 kama ilivyorekebishwa na kifungu cha sheria namba 371 cha mwaka 1942, mfuko wa akiba kwa ajili ya wafanyakazi wa serikali kifungu cha sheria namba 51yaani Provident Fund (Government Employees) Ordinance Cap 51, mfuko wa akiba ya wafanyakazi wa serikali za mitaa kifungu cha sheria namba 53 yaani Provident Fund (Local Authorities) Ordinance Cap. 53, na sheria ya malipo ya fidia ya mfanyakazi kifungu cha sheria namba 262 yaani Workmen’s Compensation Ordinance Cap 262.

Na sheria zingine zilizoudwa ni kama vile pensheni kwa ajili ya watumishi wa umma sheria namba 2 ya mwaka 1999 yaani Public Service Pension Fund (PSPF) iliyoibadili ile sheria ya Pensheni, Sura ya 371 ya mwaka 1954.; Mfuko wa bima ya afya wa taifa wa sheria namba 8 ya mwaka 1999 yaani  National Health Insurance Fund (NHIF), Mfuko wa pensheni kwa ajili watumishi wa serikali za mitaa (LAPF) chini ya kifungu cha sheria namba 9 ya mwaka 2006 na  mfuko wa akiba ya wafanyakazi wa serikali yaani Government Employees Provident (Fund GEPF) yaani utaratibu wa Hifadhi ya Jamii ulioanzishwa na Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa wafanyakazi wa serikali wasio kuwa chini ya mpango wa pensheni ulioibadili ile sheria ya Pensheni ya mwaka 1942
Kwa sasa kuna mifuko mikubwa mitano ya pensheni ya hifadhi ya jamii ambayo inatoa kinga ya hifadhi ya jamii kwa watanzania. Hiyo mifuko ni kama vile mfuko wa pensheni wa mashirika ya umma yaani Parastatal Pension Fund (PPF) ulioundwa kwa ajili ya kutoa huduma ya pensheni ya hifadhi ya jamiii kwa wafanyakazi wote wa mashirika ya umma na wa sekta ya watu binafsi na sekta ilisiyokuwa rasmi. 

Mfuko wa pensheni wa serikali za mitaa yaani Local Authorities Pensions Fund (LAPF) mfuko wa taifa wa bima ya afya yaani National Health Insurance Fund (NHIF) unaotoa huduma ya bima ya afya kwa watumishi wote wa serikali. Na mfuko wa akiba ya wafanyakazi kwa watumishi wa serikali yaani Government Employees Provident Fund (GEPF)

Jumla ya idadi ya wanachama wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii kwa Tanzania ni watu 967,573 na imegawanywa kama ifuatavyo NSSF ni 466,000, PSPF 254,559,  PPF ni 144,014, na kwa LAPF 71,000 na GEPF ni 32,000. Hii inawakilisha kama asilimia 85 ya watu wote waliajiriwa kwenye sekta iliyokuwa rasmi

Juhudi za serikali katika kutoa huduma ya kinga ya hifadhi ya jamii imeleta mafanikio makubwa ya maendeleo hapa nchini. Lakini kwa sababu sera ya hifadhi ya jamii ya kudhibiti na kusimamia bado haijaanza kutekelezwa inavyotakiwa tangia ianzishwe, udhaifu kwenye ngazi za utekelezaji, muundo, na udhaifu wa sera zilizoridhiwa na mfumo wa hifadhi ya jamii kutoka kwa wakoloni bado zinaendelea mpaka leo. Ingawa mdhibiti na msimamizi wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii yaani SSRA tangia imeanzishwa chini ya kifungu cha sheria namba 8 cha mwaka 2008 ndio inaendelea kujipanga vizuri katika utekelezaji wa usimamizi na udhibiti wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii

Taasisi za hifadhi ya jamii ya jamii nchini Tanzania zimekuwa zikiwekeza orodha ya fedha kwa faida kwenye mikopo, nyumba za kupangisha, hatifunganishi, kuweka akiba benki zote hizi zimechangia maendeleo ya kiuchumi nay a kijamii.

Kumekuweko na ongezeko kidogo sana la kuelewa juu ya mfumo wa hifadhi ya jamii hasa juu ya mafao yanayotolewa, jinsi ya kujiunga kuwa wanachama, vitega uchumi na shughuli mbalimbali za sekta. Sekta ya hifadhi ya jamii isiyo kuwa rasmi hasa kwa makundi ya kusaidiana yamekuwa yakijipanga vizuri zaidi kwa sasa ukilinganisha na hapo siku za nyuma.

Mapungufu yaliyomo kwenye mfumo huu wa hifadhi ya jamii ambayo yanahitajika kutatuliwa na sera hii ya hifadhi ya jamii yakisimamiwa na mdhitibi na msimamizi wa hifadhi ya jamii. Idadi kubwa ya watu waliomo katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni wale tu ambao wameajiriwa kwenye sekta iliyo rasmi, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu kutoka katika sekta isiyokuwa kuwa rasmi inazidi kupungua kila siku kuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii badala ya kuongezeka 

Hata hivyo inaonyesha kuwa idadi kubwa ya mafao yanayotolewa na mifuko hii ya hifadhi ya jamii nchini Tanzania yako chini ya kiwango cha shirika la kazi la dunia (ILO) yaani kwa idadi ya mafao, ubora wa mafao, na kutokwenda na ukali wa maisha ya kila siku. Mpaka sasa kuna chombo cha kudhibiti na kusimamia mashirika haya ya hifadhi ya jamii ingawa hajaanza kuleta mabadiliko. Hivyo mpaka sasa haya mashirika ya hifadhi ya jamii kila moja ina wizara yake inayoisimamia na kuwa utaratibu na kanuni tofauti za uendeshaji wa mifuko hii. Matokeo yake ni kwamba kiwango cha michango, mfumo wa mafao, na sifa za kupata mafao na hata mipako na vipa umbele vinatofautiana kabisa kwa kila mfuko.

Mpaka sasa hakuna utaratibu ulioanzishwa wa kuruhusu haki za mafao ya mwanachama kuhamishwa kutoka mfuko mmoja hadi mwingine. Matokeo yake wafanyakazi wamekuwa wakipoteza baadhi ya haki zao za mafao wakati wakihama kutoka sehemu moja ya mwajiri hadi mwajiri mwingine. Pia hii imechangia sana kuongezeka kwa tabia ya kuondoa michango ya pensheni kabla haijakomaa kiwango cha kuwa tayari kama mafao ya kustaafu. 

Baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii wanachama wanakuwa hawana haki ya mafao yao ila wanachukulia kama marupurupu. Kwa kawaida wanachama wanapoteza baadhi ya mafao yao kama wanaacha kazi kabla hawajatimiza miaka yao ya kustaafu. Na mazingira mengine haki za mafao ya mwanachama zinaaamuliwa na mwajiri kutegemeana na jinsi ya kuacha kazi haya yote ni baadhi ya changamoto za mdhibiti na msimamizi wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii kuifanyia kazi. Mpaka sasa kuna baadhi ya wafanyakazi na watumishi wa serikali wanaopata mafao au pensheni ya hifadhi ya jamii yote kutokana na kodi za mapato ya wananchi ambapo hii ni mzigo mkubwa kwa serikali hii ikiwa ni pamoja na pensheni ya viongozi wa juu serikali kama vile rais, waziri mkuu yaani specified government leaders pension scheme, pamoja pensheni za wanasiasa kama  vile wabunge yaani political leaders pension scheme.

Kumekuwa hakuna soko huru la hifadhi ya jamii ambalo linaweza kuruhusu hata taasisi za watu binafsi au sekta ya watu binafsi kuendesha mifuko ya hifadhi ya jamii kwa muda mrefu ingawa kwa sasa mdhibiti na msimamizi wa mifuko hii ametoa uhuru wafanyakazi wapya kuchagua mfuko wa hifadhi ya jamii anaoutaka pamoja na waajiri wapya kujiunga na mfuko wowote ule kulingana na kifungu namba 30 cha sheria cha mwaka 2008. Miongozo ya uwekezaji wa rasilimali za mifuko hii ya hifadhi ya jamii imeshaanza kutolewa tayari na mdhibiti na msimamizi wa hifadhi.

Christian Gaya ni Mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni. Kwa Maelezo Zaidi.
0655131341

No comments :

Post a Comment