Baadhi wa walimu wa Shule za
Sekondari wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani
waliohamishiwa shule za msingi ikiwa ni vituo vyao vipya ,wakiwa nje ya
ofisi ya halmashauri hiyo ,kupata majibu ya madai yao.
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………..
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
WALIMU 167 wa Shule za Sekondari
wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani waliohamishiwa
shule za msingi ikiwa ni vituo vyao vipya wanadai kiasi cha sh. milioni
184.5 kwa ajili ya uhamisho.
Wakizungumza na waandishi wa
habari kwenye ofisi za Halmashauri zilizopo Lugoba walimu hao walisema
walipata wakati mgumu na kushindwa kuripoti kwenye vituo vipya vya kazi
kutokana na changamoto hiyo.
Moja ya walimu aliyejitambulisha
kwa jina la Elisia Musa ,alieleza baada ya zoezi hilo kushindikana
kutokana na uhaba wa fedha waliporudi kwenye vituo vyao vya zamani
hawakupokelewa hali iliyowasababishia kuwa katika hali ya sintofahamu.
“Kutokana na kutopokelewa kwenye
vituo vyetu vya mwanzo tuliiomba halmashauri itupe barua ili iweze
kupokelewa kwenye vituo vyetu vya zamani wakati tukisubiri fedha kwenda
kwenye vituo hivyo vipya” alisema Musa.
Musa alisema, wakilipwa stahiki zao watakwenda kwenye vituo vipya vya kazi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze Edes Lukoa alielezea, walitekeleza agizo la serikali kwa kuzingatia kanuni na sheria .
Alisema walikuwa na zidio la walimu 167 wa sanaa shule za sekondari ambao walipaswa kuhamishiwa shule za msingi.
Lukoa alibainisha ,baada ya kutoa
barua walimu walikumbwa athari za kisaikolojia wakawa na uzito kwenda
kwenye vituo vyao vipya yaani kwenye shule za msingi kutokana na
kujiona kuwa ni kwanini watoke shule za sekondari wakafundishe shule za
msingi.
Alisema kuwa wakati wao
wakiendelea kuandaa malipo waliwataka walimu hao wakaripoti lakini
walichelewa kuripoti hali ambayo ili wasababisha wachelewe kufanya
malipo ya uhamisho kutokana na walimu wenyewe kuchelewesha kupeleka
madai yao.
Kwa mujibu wa Lukoa, suala kubwa
ni changamoto ya kifedha kwani jumla ya fedha wanazodai ni kiasi cha
sh. milioni 184.5 kwa ajili ya uhamisho lakini fedha halmashauri
walizonazo ni shilingi milioni 23 pekee.
Alisema , idadi ya walimu wanaotakiwa kuhamishwa ni 167 kutoka kwenye shule za sekondari 17.
Alisema kuwa zoezi hilo lilileta
mkanganyiko kwa sababu wengi wao hawakuleta viambatanisho mbalimbali
vilivyokuwa vinatakiwa ili waweze kulipwa madai yao ya uhamisho.
“Baadhi ya walimu walichelewa
kuleta nyaraka mbalimbali kutokana na wengine kupatwa na mshutuko baada
ya kuambiwa wakafundishe shule za msingi hali iliyopelekea kuwa na
ucheleweshaji wa taratibu za kuwahamisha,” alisema Lukoa.
Alisema ,watakachokifanya ni
kuwahamisha wachache kulingana na fedha zilizopo na kupeleka agenda
kwenye vikao kuomba fedha ili kuhakikisha walimu wote wanaopaswa
kuhamishiwa shule za msingi wanakwenda.
“;Kwa makubaliano na halmashauri
hatuna shida kinachotakiwa watekeleze haya tuliyoafikiana ili kusije
kukatokea kutoelewana kwa sababu sisi lengo letu ni kuwafundisha watoto
na si vinginevyo,” alisema Musa.
No comments:
Post a Comment