Pages

Sunday, July 2, 2017

Bilioni 922 Kuboresha Bandari ya Dar es Salaam.

PIX0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiweka na  mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bella Bird.
(Picha na: Frank Shija – MAELEZO)
…………………………………………………………….
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Jumla ya shilingi bilioni 922 zitatumika kwa ajili ya kuboresha bandari ya Dar es Salaam ili
kuifanya kuwa ya kisasa itakayoweza kupokea meli na shehena kubwa za mizigo kwa wakati mmoja.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameyasema hayo leo katika eneo la bandari ya Dar es Salaam alipokuwa akiweka jiwe la msingi la mradi wa uboreshaji wa bandari hiyo.
“Mradi huu utakapokamilika utainufaisha Taifa letu na nchi jirani kama vile Malawi, Zambia, Kongo, Rwanda, Uganda na Burundi ambazo zinategemea bandari yetu kusafirisha mizigo,” amesema Dkt. Magufuli.
Amesema kuwa, bandari hiyo ni lango kuu la biashara na ni kitovu cha uchumi wa nchi. Hivyo kama itaboreshwa ufanisi na uwezo wake itasaidia kukuza uchumi wa nchi kuelekea uchumi wa kati.
Aidha amesema, uboreshaji wa bandari hiyo utaondoa ucheleweshaji wa upakuaji na upakiaji wa mizigo uliokuwa ukisababishwa na ufinyu wa gati lakini baada ya kukamilika kwa upanuzi huo meli kubwa zaidi zitaweza kutia nanga.
“Mradi huu ukikamnilika utaifanya badari ya Dar es Saalam kuwa ya mfano na kutakuwa hakuna ucheleweshaji wa mizigo na itachangia maendeleo kiuchumi sio tu kwa Tanzania bali hata kwa zile nchi zitakazokuwa zinatumia bandari hii kupitisha mizigo yao” alieleza Rais Magufuli.
Aidha Rais aliuataka wa TPA kuimarisha ulinzi katika badari hiyo ili mkuifanya kuwa mahali salama pa kupitishia mizigo na kuhakikisha mizigo yote inayopita bandarini taarifa zake zinajulikana.  
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa mradi huo utanufaisha Taifa la Tanzania pamoja na nchi jirani zinazotumia bandari hiyo.
“Mradi utabadilisha ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam na kuifanya kuwa ya kisasa,” amesema Prof. Mbarawa.
Nae Mkurugunzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema kuwa uboreshaji wa bandari hiyo utaweza kuhudumia shehena ya mizigo kutoka tani milioni 14 zinazohudumiwa kwa sasa hadi kufikia tani milioni 28 na pia itaweza kuhudumia meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 320.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania, Bella Bird amesema Benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza kupitia Idara yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) itaendelea kusaidia kukua kwa Tanzania na kusaidia kuboresha maisha Tanzania.
Katika Uboreshaji wa bandari hiyo, Serikali ya Tanzania inachangia dola milioni 63.4, Benki ya Dunia Dola milioni l. 345.2 na Serikali ya Uingereza Dola milioni 12.4. Mradi unategemewa kutekelezwa katika kipindi cha miezi 36 chini ya kampuni ya China Harbour Engineering.

No comments:

Post a Comment