Pages

Friday, July 22, 2022

WAZIRI MBARAWA AWATAKA WAKANDARASI NA WAZABUNI KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEZESHAJI KUTOKA BENKI YA CRDB

 
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewataka wakandarasi na wazabuni nchini kutumia fursa za uwezeshaji zinazotolewa na Benki ya CRDB ili kuongeza ufanisi katika kazi zao, na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati nchini.

Prof. Mbalawa alisema hayo wakati akifungua Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni lililoandaliwa na Benki ya CRDB katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam. Mheshimiwa Waziri alisema fursa hizo zitasaidia kupunguza changamoto za ucheleweshwaji wa miradi mbalimbali kwasababu ya kukosekana kwa mtaji.
“Benki ya CRDB imewaletea fursa mlangoni, itumieni kupata mitaji nafuu kujijengea uwezo utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika miradi,” alisema Prof. Mbarawa huku akibainisha kuwa uwezeshaji huu unaofanywa na Benki ya CRDB utasidia kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha wakandarasi wazawa wanashiriki katika miradi (local content).

Prof. Mbalawa alipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika miradi ya ujenzi wa miondombinu mbalimbali nchini ambayo itasadia kuchochea ukuaji wa uchumi. “Tunatambua na kuthamini sana ushikiri wa Benki ya CRDB katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini, asanteni na hongereni sana,” alisema.

Prof. Mbalawa aliishauri Benki ya CRDB kupunguza riba katika mikopo ya wakandarasi kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa sekta nyengine ikiwamo ya kilimo ili kuwajengea uwezo wakandarasi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika miradi inayotekelezwa na Serikali.
“Tunawapongeza kwa mikopo hii isiyo na dhamana na maboresho mengine mliyofanya, lakini niwaombe mpunguze riba ili kutoa unafuu zaidi. Vilevile, nitoe rai kwa Wakandarasi kurejesha mikopo kwa wakati kama ilivyo katika makubaliano,” aliongezea Prof. Mbalawa huku akiishauri Benki ya CRDB kuisaidia Serikali kutoa mafunzo ya usimamizi wa miradi kwa Wakandarasi na Wazabuni.

Aidha, Prof. Mbarawa alipongeza uamuzi wa Benki ya CRDB kufungua kampuni tanzu katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akisema uamuzi huo utasaidia kufungua fursa nyingi kwa wafanyabiashara nchini ikiwamo wakandarasi na wazabuni.

“Congo kuna uhitaji mkubwa wa miundombinu ya barabara na nchi zetu zimekuwa katika mazungumzo ya namna gani tunaweza kusaidia katika kuboresha eneo hili hasa ukizingatia biashara baina ya nchi zetu inaendelea kukua”, alisema Prof. Mbalawa huku akihitimisha kwa kuipongeza Benki hiyo kwa kutunikiwa tuzo ya Benki Bora Tanzania na jarida la Euromoney la nchini Uingereza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Prof. Mbalawa kuwa Benki ya CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” imejipanga vilivyo katika kuhakikisha inashirikiana na Serikali kuboresha miundombinu nchini ili kufungua fursa za kiuchumi na kuvutia wawekezaji.

Nsekela alisema Benki ya CRDB imefanya maboresho katika huduma zake inazotoa kwa kundi hilo ambapo hivi sasa wakandarasi wakubwa na wadogo watawezeshwa kupata huduma za mikopo bila dhamana yoyote. Alisema baadhi ya huduma zilizofanyiwa maboresho ni pamoja na dhamana ya zabuni “Bid bond”, dhamana za utekelezaji wa miradi “Performance Guarantee”, dhamana za malipo ya awali “Advance Payment Guarantee”, pamoja na huduma za mikopo ya mitambo.
Nsekela aliongezea kuwa Benki hiyo pia imeboresha taratibu zake za utoaji mikopo na hivyo kuwasihi Wakandarasi kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo, kufungua akaunti, pamoja na kujiunga na huduma za bima ili kujikinga na majanga yanayoweza kutokea. “Benki ya CRDB ni Benki yenu, niwahakikishie tu sisi Tupo Tayari kuwahudumia,” alihitimisha Nsekela.

Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi na wazabuni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ukandarasi ya Gopa Contractors Tanzania Ltd, Godfrey Mogellah aliipongeza Benki ya CRDB kwa hatua hiyo ya kuwakutanisha wadau wa sekta ya ujenzi nchini huku akieleza fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB zitakwenda kuleta sura mpya katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu nchini.
 Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni nchini lililoandaliwa na Benki ya CRDB leo tarehe 21 Julai 2022 katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam.
Afisa Mkuu wa Biashara Benki ya CRDB, Boma Raballa akizungumza katika Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni nchini lililoandaliwa na Benki ya CRDB leo tarehe 21 Julai 2022 katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Kingo cha Biashara wa Benki ya CRDB, Toyi Ruvumbagu akizungumza katika Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni nchini lililoandaliwa na Benki ya CRDB leo tarehe 21 Julai 2022 katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam
Sehemu ya wakandarasi na wazabuni waliohudhuria Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni nchini lililoandaliwa na Benki ya CRDB wakifatilia mada mbalimbali leo tarehe 21 Julai 2022 katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wapili kulia), Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (kulia), Afisa Mkuu wa Biashara Benki ya CRDB, Boma Raballa (wapili kushoto), na Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile, wakiwa pamoja na baadhi ya wakandarasi na wazabuni waliohudhuria Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni nchini lililoandaliwa na Benki ya CRDB leo tarehe 21 Julai 2022 katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment