Pages

Friday, July 22, 2022

BILIONI 700 KUTUMIKA KUTEKELEZA ZOEZI LA KUHAMISHA WATU KATIKA HIFADHI NGORONGORO


Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayeshughulikia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii DK. CHRISTOPHER TIMBUKA,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22,2022 jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Janeth Raphael -Dodoma

Serikali inatarajia kutumia shilingi bilioni 700 kutekeleza zoezi la kuwahamisha wananchi wa vijiji 25 vilivyomo ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha, huku hadi sasa zaidi ya kaya 700 zenye wakazi 4344 zikiwa tayari zimejiorodhesha kwa hiari kuhamia katika kijiji cha MSOMERA, kilichopo wilayani HANDENI mkoani TANGA.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayeshughulikia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii DK. CHRISTOPHER TIMBUKA, wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23.

DK. TIMBUKA amesema kuwa kuna sababu mbalimbali zilizoisukuma serikali kuwaahamisha wananchi kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro mbali na kulinda eneo hilo ni kwamba kutokana na takwimu zilizofanywa na ofisi ya taifa ya takwimu NBS imeonekana kuwa kuna kiwango kikubwa sana cha umasikini na Asilimia kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika katika maeneo hayo kutokana na kushindwa kwenda shule kwa kuhifia wanyama wakali huku wengine wakishambuliwa na wanyama wakati wa kwenda kuchunga mifugo.

"Asilimia 64 ya wakazi wanaoishi katika hifadhi ya taifa ya Ngorongoro hawajui kusoma wala kuandika na hii inasababishwa na kuhofia kwenda shule kutokana na wanyama wakali ,huku wengine wanashindwa kufanya shughuli zao za ufugaji kutokana na kushambuliwa na wanyama wengine wanapoteza maisha kabisa"Amesema Dk.Timbuka

Kwa upande wake Msemaji mkuu wa serikali na mkurugenzi wa idara ya Habari Maelezo GERSON MSIGWA, akijibu swali kuhusiana na hatma ya wananchi waliohama kabla ya uamuzi wa serikali ya awamu ya sita wa kuhifadhi eneo la Ngorongoro lililohifadhiwa kisheria tangu mwaka 1959 amesema kuwa ni bahati kubwa kwa hawa wanaohama kwa sasa kwani serikali imewekeza fedha kubwa kwa ajili ya kuwaandalia mazingira ya kuhamia.

"Ni bahati kubwa yaani unahama alafu unakuta nyumba ipo kwenye eneo la ekari mbili na nusu alafu una shamba la ekari tano umepewa bure na serikali yako sikufu inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan tuseme tu kwamba hawa wananchi wa Ngorongoro wana bahati kubwa na niwaombe tu watumie hii bahati vizuri"Amesema Msigwa

No comments:

Post a Comment