SERIKALI imeokoa Sh. bilioni 249 zilizokuwa zitumike kugharamia wagonjwa kwenda nje ya nchi kufuata huduma za matibabu ambazo awali zilikuwa hazipatikani hapa nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Profesa Abel Makubi ametoa taarifa hiyo jijini dodoma wakati wa mahojiano maalum yaliyofanywa na kitengo cha elimu ya afya kwa umma cha Wizara ya Afya ambapo amesema katika kipindi cha nyuma takribani wagonjwa 58,000 walikuwa wanapata rufaa za kwenda nje na kugharimu Sh. bilioni 374 lakini kwa sasa wanatibiwa hapa nchini ambapo serikali inatumia Sh. Bilioni 125.3.
Aidha Prof.Makubi amesema unafuu huo umetokana na u oboreshaji mkubwa wa miundombinu katika hospitali za rufaa na hospitali maalum uliofanywa na serikali kwa kuweka vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuwa na madaktari bingwa kila hospitali za rufaa na maalum pamoja na zile za kanda
Amezitaja hospitali hizo kuwa ni hospitali ya taifa muhimbili, Moi, Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Kibong'oto Milembe na za kanda ni Mbeya, Benjamin mkapa, Kcmc,Bugando, Chato na Mtwara.
Akizungumzia hali ya utoaji chanjo inavyoendelea hapa nchini Prof. Makubi amesema zaidi ya watu milioni 2 wamechanja na kwamba uhamasishaji unaendelea kufanyika kuanzia ngazi ya jamii na mwitikio kwa sasa ni mkubwa ikilinganishwa na awali.
Aidha ameongeza kuwa utoaji chanjo siyo wa kulazimishana isipokuwa elimu itolewe kwenye mitaa ili kila mwananchi aelewe na akubali kwa hiari yake kuchanja.
Prof.Makubi ametoa mwito kwa watu wote ambao walichoma chanjo ambazo zinahitaji dozi mbili kwenda kuchoma dozi ya pili kwani ili chanjo ikamilike lazima umalize dozi.
No comments:
Post a Comment