Pages

Wednesday, February 2, 2022

SERIKALI KUPIMA UTENDAJI KAZI WA TAASISI ZAKE KIELEKTRONIKI - WAZIRI JENISTA


Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inaboresha Mfumo wa Uwazi wa Kupima Utendaji Kazi wa Taasisi unaojulikana kama Mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi katika ngazi ya Taasisi za Umma kuwa wa kielektroniki ili utumike kupima utendaji kazi wa taasisi za umma nchini.

Akizungumza ofisini kwake Jijini Dodoma, Mhe. Jenista amesema, mfumo huo wa kielektroniki utawezesha makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi za Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Malengo yaliyomo ndani ya Mkataba yatakuwa na vigezo, shabaha na viashiria vitakavyotumika kupima utendaji kazi wa Taasisi kila mwisho wa mwaka. Mkataba huu unalenga kuimarisha dhana ya utendaji unaojali matokeo, kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, na kuongeza uwajibikaji wa viongozi katika Taasisi za Umma,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, Mfumo huo wa kielektroniki ukikamilika utatumika kulinganisha na kushindanisha utendaji wa taasisi na kutoa tuzo za utendaji bora kwa taasisi zenye utendaji mzuri kila mwaka.

Akizungumzia faida za Mfumo huo, Mhe. Jenista amesema utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa Sera, Mikakati na Vipaumbele vya Taasisi, Sekta na Taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa umma, kuimarisha utamaduni wa utendaji unaojali matokeo na kuleta matumizi bora ya rasilimali za Umma.

Aidha, Mhe. Jenista amewataka Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma kuendelea kusimamia utekelezaji wa mfumo huu kikamilifu na wahakikishe wanatenga bajeti kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wake katika Taasisi wanazoziongoza.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga vizuri kujenga na kusimamia mifumo yenye tija kupitia sekta ya Utumishi wa Umma.

No comments:

Post a Comment