(PICHA NA BODI YA MIKOPO- HESLB)
*********************************
- Sasa mfumo kufungwa Septemba 10 badala ya Agosti 31
- TZS 464 bilioni zatengwa kwa ajili ya wanafunzi 145,000
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
- Agosti, 2020
Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuongeza muda wa
siku kumi za kuomba mkopo kuanzia kesho (Jumanne, Septemba 1, 2020) ili
kuwawezesha wanafunzi waombaji mkopo ambao hawajakamilisha maombi yao ya
kukamilisha.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amewaambia wanahabari jijini Dar es
salaam leo (Jumatatu, Agosti 31, 2020) kuwa uamuzi huo unafuatia maoni,
ushauri na maombi kutoka kwa wanafunzi, wazazi na walezi ambao HESLB
imepokea.
Maombi yaliyopokelewa hadi sasa
“Hadi leo
asubuhi, tumeshapokea maombi 85,921 kwa njia ya mtandao, na kati ya
hayo, maombi 71,888 sawa na asilimia 84 ni kamilifu na yana nyaraka
muhimu na mengine 14,033 yanakosa nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa
au vya vifo vya wazazi wa waombaji ambavyo havijathibitishwa na RITA au
Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar maarufu kama ZCSRA,”
amesema Badru.
Badru
ameongeza kuwa HESLB imeendesha programu za elimu ya uombaji mkopo kwa
usahihi kwa wanafunzi katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar
pamoja na kwenye kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako
wamepokea maoni na maombi ya kuongezwa kwa muda na kutoa nafasi kwa
wanafunzi waliopo kwenye kambi za JKT kuomba mkopo mara wamalizapo
mafunzo.
“Kuhusu
waliopo JKT hivi sasa, tunaendelea kuwasiliana na Makao makuu ya JKT
ambao tunashirikiana kuhakikisha vijana wote wahitaji wanapata fursa
bila kuathiri mafunzo ambayo ni muhimu,” amesema Badru.
Bajeti ya Mikopo kwa 2020/2021
Kuhusu bajeti ya
fedha za mikopo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema katika mwaka wa masomo
2020/2021, Serikali imetenga TZS 464 bilioni kwa ajili ya wanafunzi
145,000 wa taasisi za elimu ya juu na kati yao, 54,000 wanatarajiwa kuwa
ni wa mwaka wa kwanza.
“Hili ni
ongezeko la kutoka jumla ya TZS 450 bilioni zilizotolewa mwaka huu
2019/2020 ambazo zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 132,292 hadi sasa,”
amesema Badru katika mkutano uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka RITA na
Shirika la Posta Tanzania (TPC), taasisi zinazowahudumia waombaji
mkopo.
Ushauri wa RITA na Posta
Akiongea katika
mkutano huo, Meneja Masoko wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi
(RITA) Josephat Kimaro amewakumbusha wanafunzi waombaji mkopo
waliowasilisha maombi ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya
wazazi wao, kufungua barua pepe walizotumia kuwasilisha maombi yao RITA
ili kupokea majibu.
Naye Meneja
Mkuu anayesimamia Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC)
Mwanaisha Said amesema wamekubaliana na HESLB kuendelea kupokea nakala
ngumu za maombi ya mikopo katika ofisi za TPC nchini kote na
kuziwasilisha HESLB hadi Septemba 15 na kuwataka wanafunzi kutokuwa na
wasiwasi na kutokupokelewa kwa bahasha zao.
No comments:
Post a Comment