Mkurugenzi wa Utawala na
rasilimali Watu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Victor Katagere akizungumza
na Watumishi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART katika Kikao kazi
cha taasisi zilizoko chini ya Wizara yake Kwenye Ofisi za Wakala Ubungo
Maji Jijini Dar es Salaam Juni mosi 2020.Mtendaji
Mkuu wa DART Ronald Lwakatare akitoa maelezo ya utangulizi kwa
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw.
Victor Kategere kabla ya kuzungumza na Watumishi wa Wakala Jijini Dar
es Salaam Juni mosi 2020.
*********************************
Na. Mwandishi Wetu, DART.
Watumishi wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART), wametakiwa kufanya kazi kwa
bidii, weledi na
kujituma ili kufanikisha ndoto za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli za kuwa na Tanzania mpya.
Maagizo hayo yametolewa Jijini Dar
es Salaam na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Ofisi ya Rais
TAMISEMI Bw.Victor Kategere, alipozungumza na Watumishi wa Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwenye kikao kazi cha kukumbushana
majukumu ya utendaji kwa watumishi wa umma wa taasisi zilizoko chini ya
Wizara hiyo.
Amesema DART ni taasisi muhimu
sana ambayo inategemewa katika kupunguza changamoto za msongamano na
foleni katika Jiji la Dar es Salaam, hivyo ni wajibu wa watumishi
kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa.
“Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
zaidi ya milioni 6 wote wanawatazama na wanamatarajio makubwa sana kwenu
katika kuwapatia huduma ili hatimaye shughuli zao za maendeleo
zirahisishwe, hivyo uwepo wetu katika taasisi hii na Serikali kwa ujumla
ni wa maana” Alisema Kategere.
Aidha aliwaasa watumishi kuendelea
kufuata Sheria Kanuni na taratibu zote za utumishi wa umma, hasa suala
la kutunza na kuhifadhi siri za Serikali kwani kumejitokeza baadhi ya
watumishi wasio waaminifu ambao wamekua wakitoa nyaraka nyeti na za siri
kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo si sawa.
“Maadili yanakataza kabisa kwa
watumishi kutoa nyaraka nyeti za Serikali mitandaoni na hata kwa watu
ambao haziwahusu , jambo ambalo ni hatari sana kwa mustakabali wa
Taasisi na nchi kwa ujumla” Alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kategere alisema kuwa, utendaji
kazi kwa watumishi wa umma kwa nyakati hizi unatakiwa uwe wenye tija na
unaotoa matokeo chanya hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inafanya
mageuzi makubwa kwenye miundombinu kuelekea Tanzania ya Viwanda.
Vilevile amesema ameridhishwa na
maandalizi ya mfumo mpya wa Tehama ambao utasaidia katika ukusanyaji wa
mapato kwa njia ya kielektroniki, hivyo akasisitiza umuhimu wa DART
kuendelea kuwa wabunifu ikizingatiwa kwamba dunia sasa inaendelea kukua
kimaendeleo ambapo mambo mengi yanafanyika kidijitali.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
DART Mhandisi Ronald Lwakatare, akizungumza katika kikao hicho amesema
Wakala unaendelea na usanifu na ujenzi wa miradi ya barabara za Mabasi
Yaendayo Haraka katika Barabara ya Kilwa kuelekea Mbagala na matarajio
ni kuendelea kupanua mtandao kuelekea katika maeneo mengine kadiri
bajeti itakavyoruhusu.
“Tunaendelea na ujenzi wa
miundombinu katika maeneo mengine ya Jiji na lengo letu ni kuhakikisha
kule kote ambako tumefanya utafiti na kujiridhisha kunafaa kuwa na
barabara ya mwendokasi tunapeleka huduma hiyo” Alisema Mhandisi
Lwakatare.
Amesema kuwa Taasisi yake
inajipanga pia kuhakikisha inafanya utafiti katika Jiji la Dodoma ambalo
ndio makao Makuu ya Nchi kuona ni barabara zipi zitafaa kwa ajili ya
kujenga miundombinu ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka.
“Nilimsikia Mh.Rais wakati wa
uzinduzi wa jengo la Tarura kuwa anatamani Jiji la Dodoma liwe na
barabara za mabasi yaendayo haraka pamoja na treni za haraka, sisi
tumelichukua na tunajipanga ili wataalam wetu waende angalau kwa kuanzia
kutathmini nini cha kufanya ili kama jukumu hilo tutakabidhiwa
tulitekeleze kwa kiwango cha hali ya juu” Alisema.
Awali akimkaribisha Bw. Kategere,
Mhandisi Lwakatare alisema janga la ugonjwa wa Corona lilisababisha
hasara kubwa katika uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka kwani zaidi ya
asilimia 70 ya mapato hayakupatikana kutokana na utaratibu wa kubeba
abiria kulingana na idadi ya viti vilivyomo kwenye basi.
Alisema uwezo wa mabasi ni kubeba
abiria 140 lakini idadi ya viti ni 40 tu hivyo unakuta uendeshaji
unakuwa wa hasara kwani mabasi hayo ya haraka yamebuniwa kubeba abiria
waliosimama zaidi ya wale waliokaa.
Mhandisi Lwakatare alibainisha
kuwa, mipango ya kuimarisha usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka inaendelea
vyema na mwishoni mwa mwaka huu ana imani mzabuni aliyepewa kazi ya
kununua mabasi atakamilisha kazi hiyo ili hatimaye kuwa na mabasi ya
kutosha kwa ajili ya kurahisisha usafiri Jijini Dar es Salaam.
Aidha alisema kuwa umuhimu wa
kuongeza idadi ya mabasi umekua mkubwa kutokana na kuongezeka kwa
watumiaji wa usafiri huo, kwani wakati mradi unaanza ulikua unahudumia
watu 70,000 kwa siku ambao kwa sasa wameongezeka hadi kufikia 200,000
kwa siku.
Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka –
DART ni Taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, yenye jukumu la
kusimamia na kuendeleza miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka katika
Jiji la Dar es Salaam.Taasisi nyingine zilizoko chini ya TAMISEMI ni
pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu, Bodi ya Mikopo ya Serikali za
Mitaa,Tarura, Shirika la Masoko Kariakoo,Chuo cha Serikali za Mitaa
Hombolo pamoja na Shirika la Elimu Kibaha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment