Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifafanua jambo mbele ya Mkuu
wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo (kushoto) akiwa katika ofisi ya ardhi
mkoa wa Rukwa baada ya kuizindua rasmi jana. Wa pili kulia ni Kamishna
Msaidizi wa ardhi mkoa wa Rukwa Swagile Msananga na wa tatu kulia ni
Katibu Tawala mkoa wa Rukwa Benard Makali.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akielekea kukagua ofisi za ardhi
mkoa wa Rukwa baada ya kuizindua jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu
wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya
Sumbawanga Dkt Khalfan Haule na kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa
wa Rukwa Swagile Msananga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia baadhi ya vifaa vya
upimaji vilivyopo katika ofisi ya ardhi mkoa wa Rukwa baada ya kuizindua
jana. Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo na wa pili kulia
ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Rukwa Swagile Msananga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa baadhi ya sehemu
zinazofanyiwa ukarabati katika ofisi ya Baraza la Ardhi la Nyumba la
wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Said Mtanda
jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa
Namanyele wilayani Nkasi alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa
ofisi ya baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Nkasi jana. Kulia kwa
Naibu Waziri ni Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo.
Sehemu ya wananchi wa Namanyele
wilaya ya Nkasi mkoa wa Rukwa waliojitokeza kumpokea Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda
kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Baraza la Ardhi la Wilaya na
Nyumba la Nkasi mkoani Rukwa jana. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA
YA ARDHI)
…………………………………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM SUMBAWANGA
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaagiza
Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika ofisi za mikoa kukaa na taasisi za
serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi kuangalia namna bora ya
kulipa madeni wanayodaiwa.
Dkt Mabula alitoa
agizo hilo jana mkoani Rukwa wakati akizundua rasmi ofisi ya ardhi ya
mkoa ikiwa ni mfululilizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa
mbalimbali nchini. Tayari ofisi saba za ardhi katika mikoa ya Tanga,
Arusha, Manyara, Singida, Iringa, Njombe na Songwe zimezinduliwa.
Alisema, mkoa wa
Rukwa una taasisi za serikali pamoja na watu binafsi ambao kwa ujumla
wao wanadaiwa zaidi ya shilingi bilioni moja kiasi alichokieleza kuwa ni
kikubwa na fedha yake ingeweza kutumika katika shughuli za maendekeo
kama vile ujenzi wa hospitali au barabara.
Alizitaja baadhi
ya taasisi za serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa
Rukwa kuwa ni pamoja na Shirika la umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo Kikuu Huria na
kubainisha kuwa katika kumuwezesha rais kufanya kazi ya shughuli za
maendeleo kuna wajibu wa kulipa kodi ya pango la ardhi.
‘’Bilioni moja ni
fedha nyingi sana nawaagiza Makamishna Wasaidizi wa mikoa kukutana na
taasisi pamoja na watu wengine wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi
kukubaliana namna bora ya kulipa fedha wanazodaiwa vinginevyo taratibu
za kisheria zitafuata’’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Taasisi za serikali
zinatenga fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya kulipia gharama
mbalimbali ikiwemo kodi ya pango la ardhi na kutolipa kodi hiyo ni
kutotimiza wajibu wa kulipa kodi ya ardhi.
Alisema, Wizara
yake ilikutana na makampuni na taasisi za serikali zenye malimbikizo
makubwa ya kodi ya pango la ardhi mkoani Dodoma na baada ya kukutana
ndani ya mwezi mmoja zilikusanywa takriban bilioni ishirini na moja
jambo linaloonesha kuwa taasisi hizo zinazo fedha kwa ajili ya kodi
hiyo.
Katika hatua
nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt
Angeline Mabula alisema, wizara yake imeridhia kuanzishwa Baraza la
Ardhi la Nyumba la wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Hatua hiyo
inafuatia Dkt Mabula kuridhishwa na juhudi za wilaya ya Nkasi katika
kuanzisha baraza hilo ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi yake
katika eneo la Namanyele wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa na kusema kuwa kwa
sasa takriban mabaraza mia moja ya ardhi ya nyumba ya wilaya
yameidhinishwa lakini ni mabaraza 55 ndiyo yanayofanya kazi.
Hata hivyo,
aliongeza kwa kusema kuwa, wakati mchakato wa ofisi za baraza hilo
ukiendelea mwenyekiti wa baraza la ardhi la wilaya ya Sumbawanga anaweza
kupanga ratiba na kwenda kuendesha mashauri ya migogoro ya ardhi kwenye
wilaya ya Nkasi kwa lengo la kupunguza mashauri hao.
Mkuu wa mkoa wa
Rukwa Joachim Wangabo alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kuwa, mkoa wake una baraza moja tu la ardhi la
nyumba na wilaya huku mkoa mzima ukiwa umesajili jumla ya mashauri 308
ya migogoro ya ardhi kuanzia mwezi januari hadi juni mwaka huu.
Alisema, kufuatia
hali hiyo iko haja ya kuanzishwa baraza la ardhi la wilaya ya Nkasi kwa
kuwa wananchi wa wilaya hiyo wamkuwa wakipata taabu kutembea umbali
mrefu na wakati mwingine hulazimika kusafiri kilomita 160 kufuata huduma
ya baraza wilayani Sumbawanga.
No comments:
Post a Comment