Pages

Monday, June 1, 2020

MRADI WA KWANZA KUTUMIA CHANZO CHA MAJI YA MTO KAGERA WAANZA KUTEKELEZWA



Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kyaka, Lubale na Katuntu Wilayani Missenyi (hawapo pichani) wakati wa kukabidhi kwa Mkandarasi eneo la mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi na Diwani wa Kata ya Kyaka, Projestus Tegamaisho
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (mbele katikati) alipowasili katika Kijiji cha Kyaka kwenye eneo litalojengwa chanzo cha Maji cha Mradi wa Kyaka Bunazi wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akielekea kwenye eneo litalojengwa chanzo cha mradi wa Maji Kyaka Bunazi wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele ambaye ni msimamizi wa utekelezaji wa mradi wa Maji wa kyaka Bunazi kwa niaba ya Wizara ya Maji akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. kitila Mkumbo (hayupo pichani)
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akiwasili katika Kijiji cha Kyaka wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka Bunazi. Kutoka kushoto Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kagera, Mhandisi Warioba Sanya.
Mkurugenzi, Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (aliyesimama) akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kyaka, Lubale na Katuntu Wilayani Missenyi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka Bunazi.
……………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amezindua na kukabidhi rasmi ujenzi wa mradi wa kwanza nchini utakaotumia maji kutoka Mto Kagera maarufu kama Mradi wa
Maji wa Kyaka Bunazi utakaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 15.1.
Uzinduzi kwa ajili ya kuanza kwa utekelezwaji wa ujenzi wa mradi umefanyika Juni 1, 2020 Wilayani Missenyi Mkoani Kagera na kushuhudiwa na wananchi kutoka vijiji mbalimbali wilayani humo ambapo Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering and Construction Corporation (CCECC) alikabidhiwa rasmi eneo la mradi kwa ajili ya kuanza mara moja utekelezaji wake.
Profesa Mkumbo alipongeza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kutumia Mto Kagera kuwapatia wananchi maji safi na salama na huku akibainisha kwamba mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi ni wa kwanza nchini utakaotumia Mto Kagera kama chanzo chake cha maji kwa wanachi wanaouzunguka.
“Mradi huu ni wa kwanza kutumia maji ya Mto Kagera kupelekea huduma ya maji kwa wananchi, kwani hatukuwahi kuwa na mradi wa namna hii ila kwa Awamu hii ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli hili limewezekana,” alibainisha Profesa Mkumbo.
Akielezea namna ambavyo mradi huo ulivyopatikana, Profesa Mkumbo alisema ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Julai 11, 2019 la kuhakikisha wananchi wa Mji wa Kyaka wanapata huduma ya majisafi kutoka Mto Kagera baada ya kujionea kero ya maji waliyokuwa nayo. 
“Rais Dkt. Magufuli alimuelekeza Waziri wetu wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha anafika hapa ili kuhakikisha tatizo la Maji linatatuliwa haraka na kesho yake Waziri alifika na alituelekeza sisi wasaidizi wake tuanze utekelezaji wa mradi mara moja,” alisema Profesa Mkumbo.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika sehemu mbili ambapo moja itatekelezwa na Kampuni ya CCECC kwa gharama ya shilingi bilioni 9.4 na nyingine itatekelezwa na wataalam wa ndani kwa gharama ya shilingi bilioni 5.7.
Alifafanua kuwa utaratibu wa kutekeleza baadhi ya miradi kwa kutumia wataalam wa ndani ulianzishwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa na umeonyesha mafanikio makubwa kwani umewezesha kupatikana kwa miradi mizuri na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na utumiaji wa wakandarasi. 
“Mheshimiwa Waziri alianzisha mfumo huu unaitwa force account kabla ya hapo ilikua hata shughuli ndogo anatafutwa mkandarasi lakini sasa shughuli nyingi za kawaida zinatekelezwa na wataalam wetu wa ndani na imetusaidia kuokoa fedha nyingi,” alisema Profesa Mkumbo.
Aidha, alibainisha kuwa mradi unatekelezwa kwa fedha za ndani na kwamba tayari fedha zimetengwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati huku akiweka wazi kwamba shilingi milioni 650 ilikwishatolewa kwa ajili ya utekelezaji wake.
Profesa Mkumbo alielekeza mradi ukamilike kwa wakati kwani hakuna kikwazo cha fedha kwenye utekelezaji wake na pia wahakikishe shughuli zinazoweza kufanywa na wananchi wa maeneo ya mradi zifanywe na wananchi hao. 
“Sisi kama Wizara tumejipanga; fedha ipo Mkandarasi hata akileta kesho maombi yake ya awali analipwa, hakuna kikwazo cha fedha kwenye kutekeleza mradi huu,” alisisitiza.
Akizungumzia hali ya utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini, Profesa Mkumbo alibainisha kwamba Mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi unakuwa ni mradi wa 1,425 miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwenye Serikali ya Awamu ya Tano.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa miradi 792 imekamilika na kwamba miradi 633 inaendelea kutekelezwa huku miradi 41 ikitekelezwa kwa fedha za nje na mingine yote iliyobakia ikiwa inatekelezwa kwa fedha za ndani.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele ambaye ndiyo msimamizi wa utekelezaji wa mradi kwa niaba ya Wizara ya Maji alisema sehemu itakayotekelezwa na Mkandarasi CCECC itahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa kituo cha tiba ya maji, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye kituo cha tiba ya maji lenye urefu wa kilomita 1.5 na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji yaliyotibiwa la lita milioni mbili.
Aliongeza kuwa sehemu ya pili ya mradi itahusisha ulazaji wa bomba kuu la usambazaji kutoka kwenye tenki lenye urefu wa kilomita 14 na ulazaji wa mtandao wa bomba za kusambaza maji kwa wananchi ambayo itatekelezwa na wataalam wa ndani kutoka Wizara ya Maji, Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA), Mamlaka ya Maji Bukoba (BUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).
Mhandisi Msenyele alisema mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Julai, 2021 na kwamba kukamilika kwake kutawezesha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Kyaka, Bunazi pamoja na maeneo jirani kwa asilimia mia moja na hivyo kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji inayowakabili wananchi wa maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment