………………………………………………………………….
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za
rambirambi kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai na wananchi wa Jimbo la Sumve Mkoani
Mwanza kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Richard Mganga
Ndassa.
Mhe. Ndassa amefariki dunia ghafla leo tarehe 29 Aprili, 2020 Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amesema “Nimesikitishwa
na taarifa za kifo cha ghafla cha Mhe. Ndassa, nakumbuka mimi na yeye
tulianza pamoja Ubunge mwaka 1995, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Sumve
na mimi nikiwa mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki ambalo sasa hivi
linaitwa Jimbo la Chato, namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali
pema peponi, Amina”
Mhe. Rais
Magufuli amemuomba Spika, Mhe. Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa
familia ya Marehemu, Wabunge, wananchi wa Sumve pamoja na ndugu, jamaa
na marafiki wote walioguswa na kifo cha Mhe. Ndassa.
Amewataka wafiwa
wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi
hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
29 Aprili, 2020
No comments:
Post a Comment