Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC,
Anna Henga (katikati) akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Ripoti ya
Haki za Binadamu Tanzania 2019. Uzinduzi huo uliofanyika leo Aprili
29, 2020 katika ofisi za LHRC jijini Dar es Salaam na wadau kufuatilia
kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Anna Henga (katikati), Afisa Utafiti, Fundikila
Wazambi (kushoto) na Mkurugenzi wa Uwajibikaji na Uwezeshaji wa Kituo
hicho, Felista Mauya (kulia) wakionesha nakala za Ripoti ya Haki za
Binadamu Tanzania 2019 mara baada ya uzinduzi leo Jumatano leo Aprili
29, 2020 katika ofisi za LHRC jijini Dar es Salaam na wadau kufuatilia
kwa njia ya mtandao.
***
Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) kimezindua Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2019
inayoangazia hali ya haki za binadamu kwa mwaka 2019 na kufanya
ulinganisho wa hali ilivyokuwa mwaka 2018.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano, Aprili 29, 2020 kwa njia ya mtandao kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC amesema ripoti hiyo inahusisha matukio
ya ukiukwaji wa haki za binadamu sambamba na mapendekezo kwa ajili ya
uboreshaji wa sera, sheria na utendaji katika jamii.
Anna amesema ripoti hiyo
inaangazia hali ya haki za binadamu katika nyanja za haki za kiraia na
kisiasa; haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni; haki za makundi
yaliyo hatarini; mifumo ya Ulinzi wa Haki za binadamu na haki za
kijumla.
“Ripoti hii ni matokeo ya
taarifa mbalimbali zilizokusanywa na LHRC ikiwemo taarifa kutoka kwa
waangalizi wa haki za binadamu walio nchi nzima, wasaidizi wa kisheria
walio katika wilaya mbalimbali, taarifa rasmi toka taasisi za Serikali,
Bunge, Mahakama, jeshi la polisi, vyombo vya habari na asasi mbalimbali
za kiraia zisizo za Serikali. Taarifa hii pia hutumia taarifa mbalimbali
za kitaifa lakini pia na za kimataifa, hasa zinazolenga kuelezea hali
ya haki za binadamu nchini”, amesema Anna Henga.
Kwa mujibu wa Ripoti hiyo, haki tano zilizokiukwa zaidi kwa mwaka 2019 ni pamoja na:
Haki ya Kuishi ambapo matukio
kama vile mauaji ya wanawake, mauaji ya watoto, mauaji yanayotokana na
kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayotokana na imani za kishirikina
pia yameendelea kuripotiwa.
Uhuru dhidi ya ukatili; ambapo
matukio yaliyoripotiwa ni Ukatili wa kingono na kimwili dhidi ya watoto;
ukatili wa kingono na kimwili dhidi ya wanawake. Katika kipindi cha
kuanzia mwaka 2017 hadi mwezi Juni 2019, jumla ya matukio 88,612 ya
ukatili wa kijinsia yameripotiwa.Matukio ya ukatili wa
kingono dhidi ya watoto jumla ya matukio 3,709 ya ubakaji yaliripotiwa
katika vituo vya polisi nchini ikiwa ni matukio 126 zaidi ya yale
yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2018. ukatili dhidi ya
watu wenye ulemavu na wazee nao umeendelea kushika kasi katika tukio
moja, bibi wa miaka aliripotiwa kubakwa hadi kufariki.
Uhuru wa Kujieleza; muendelezo
wa uminywaji wa uhuru wa kujieleza ambapo kumekuwepo na Sheria
kandamizi, ukamataji na uwekaji kizuizini waandishi wa habari kinyume na
sheria pamoja na kufungiwa kwa vyombo vya habari.
Haki ya kuwa Huru na Salama;
Ripoti imeripoti matukio kadhaa yanayopelekea kuminywa kwa haki hiyo
kama vile Mashambulizi na mauaji ya madereva bodaboda pamoja na Matukio
ya utekaji, watu waliopotea na matukio ya ukamataji na uwekaji kizuizini
kinyume na sheria.
Haki ya Kujumuika na
Kukusanyika; zimeendelea kukiukwa hasa kipindi hiki ambapo tunaelekea
uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Vyama vya siasa, hususan vya upinzani,
viliendelea kulalamikia maamuzi haya kwamba yanakiuka haki yao
inayolindwa na Katiba, jambo linaloathiri pia ushindani wao kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Vyama hivi pia vililalamika kwamba
marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa yanaminya uhuru wao wa
kujumuika na kukusanyika.
LHRC kupitia Mkurugenzi Mtendaji
wake, Anna Henga wametoa rai kwa serikali na wanajamii kwa ujumla
kuchukua hatua katika kulinda na kudumisha haki za binadamu.
“Tunatoa rai kwa serikali,
taasisi na jamii ya Watanzania kuendelea kulinda haki za binadamu na
kuwawajibisha wale ambao wameshindwa kuheshimu haki hizo bila ubaguzi wa
kikabila, kidini, kisiasa na kijinsia ili tuweze kuifikia jamii yenye
haki na usawa”,amesisitiza Anna Henga.
Ripoti ya Haki za Binadamu
Tanzania 2019 ni muendelezo wa ripoti za kituo hicho zinazotolewa kila
mwaka kwa lengo la kuonesha hali na kutoa mapendekezo ya maboresho.
No comments:
Post a Comment