Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipofungua kitengo cha kuchuja
damu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, Machi 1,
2020. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, wa tatu kulia ni
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu na wa pili kulia ni Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt.
Naima Yusuf. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Christopher Nyange mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika
kitengo cha kuchuja damu baada ya kufungua kitengo hicho katika
hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mganga ya Bombo, Machi 1, 2020. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akifungua kitengo cha kuchuja damu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Tanga ya Bombo, Machi 1, 2020. Wa tatu kushoto ni Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kushoto ni
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Mwita Waitara na
kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
***************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amefungua mradi wa huduma ya kuchuja damu katika
hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo na kupunguza gharama ya kuwasafirisha wagonjwa wenye matatizo ya figo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuata hiduma hiyo.
hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo na kupunguza gharama ya kuwasafirisha wagonjwa wenye matatizo ya figo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuata hiduma hiyo.
Pia, Waziri Mkuu
amefungua mradi wa ujenzi wa barabara ya Makorora-Msambweni (km nne)
iliyojengwa kwa thamani ya sh. bilioni 5.9 ambayo itarahisisha
mawasiliano kwa wakazi wa kata za Msambweni, Makorora, Mzingani na
watumiaji wengine wa barabara hiyo.
Waziri Mkuu
amezindua miradi hiyo kwa nyakati tofauti jana (Jumapili, Machi 1, 2020)
wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Tanga,
ambapo alisisitiza azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi wote.
Alisema sekta ya
afya imepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka minne iliyopita na
Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na
maboresho ya stahili za watumishi. Amewataka watumishi waendelee kuwa
watulivu wawe na Imani na Serikali yao.
Alisema ni vema
kwa watumishi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanafanyakazi kwa uaminifu
na uadilifu ili wagonjwa wenye matatizo ya figo pamoja na matatizo
mengine ya kiafya wapate huduma bora bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Pia, Waziri Mkuu
aliwataka watumishi hao kuandaa utaratibu wa kutoa elimu kila siku
asubuhi juu ya umuhimu wa kujikinga na magonjwa yanayoambukiza
na yasiyoambukiza ambayo ni hatari na ya gharama kubwa.
“Suala la mazoezi
ni tiba muhimu na nyie wataalamu ambao mnajua ugonjwa huu tunautibu
vipi ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, hivyo andaeni nafasi ya dakika
tano hadi kumi za kutoa elimu na kuhamasisha watu wajenge tabia ya
kufanya mazoezi. Magonjwa mengine yanaweza kutibika kwa kufanya mazoezi
na kubadilisha mitindo ya maisha.”
Waziri Mkuu
alisema Serikali imeboresha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi
wake zikiwemo za afya, hivyo aliwaagiza viongozi katika ngazi mbalimbali
wahakikishe hakuna mwananchi anayekwenda kwenye maeneo ya kutolea
huduma na kukosa dawa au vipimo.
Akizungumza
kuhusu barabara ya Makorora-Msambweni, Waziri Mkuu alisema mbali na
kurahisisha mawasiliano pia itaboresha usalama na mazingira ya wananchi
kutokana na uwepo wa taa za barabarani jambo litakaloongeza thamani ya
makazi.
Awali, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema
huduma za figo nchini zilikuwa zinatolewa katika vituo 19 vya binafsi na
hospitali tano za Serikali ambazo ni Hospitali za Kanda za Rufaa
Muhimbili, Mbeya, Bugando, KCMC na Benjamin Makapa.
Waziri Ummy
alisema hadi 2016 asilimia 90 ya huduma za kusafisha figo zilikuwa
zinatolewa na sekta binafsi na asilimia 10 taasisi za umma. “Hali hii
inasababisha huduma za usafishaji figo kuwa na gharama kubwa na kukosa
uwiano wa huduma hasa kwa wananchi waishio mikoa ya pembezoni.”
Alisema Serikali
imepanga kutanua huduma hizo ili ziweze kutolewa katika hospitali zote
za rufaa za mikoa, ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo
imeanza kwa hospitali za rufaa za mikoa ya minane ambazo ni Bombo-Tanga,
Meru-Arusha, Mtwara, Iringa, Bukoba-Kagera, Maweni-Kigoma na
Sekoutoure-Mwanza.
Waziri Ummy
alisema uanzishwaji wa kituo kimoja cha kutolea huduma ya kuchujia damu
hadi kuanza kufanya kazi kama kilivyo cha Bombo kinagharimu sh milioni
574,794,177, hivyo kwa vituo hivyo nane ambavyo mwezi huu vinataanza
kutoa huduma vitagharimu sh. bilioni 4.5.
Kwa upande
wao,wagonjwa wenye matatizo ya figo waliishukuru Serikali kwa
kuwasogezea huduma ya kuchuja damu katika hositali ya Rufaa ya mkoa wa
Tanga kwa kuwa awali walilazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma
hiyo katika hospitali ya Muhimbili.
Pia, Wagonjwa hao
licha ya kuishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma, pia wameiomba
iangalie uwezekano wa kupunguza gharama ili watu wengi waweze kumudu
matibabu hayo kwani kwa sasa gharama ya session moja ni sh. 250,000.
No comments:
Post a Comment